MWENYEKITI wa Wazazi Wilaya ya Babati Vijijini, Willy Bayo,
amesema matokeo mabaya kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka
jana yametokana na mitaala mibovu ya kufundishia pamoja na kuzibwa kwa
mianya ya uvujaji wa mitihani iliyokuwa ikifanywa na baadhi ya walimu
nchini.
Bayo alitoa kauli hiyo juzi wakati akichangia mada kwenye kikao cha
wadau wa elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Manyara,
kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo.
Alisema pamoja na matokeo hayo kuwa ni janga la kitaifa inapaswa
serikali ielewe kwamba tatizo hilo limechangiwa na kuzibwa na
kudhibitiwa kwa uvujaji wa mitihani uliokuwa ukifanywa na baadhi ya
walimu kwenda kwa watahiniwa nchini.
Alibainisha kwamba tegemeo la kuvuja kwa mitihani kuliwafanya pia
walimu kutokuwa na ari ya kufanya kazi kwa kutegemea kuwa mwisho wa
masomo mwanafunzi atafaulu kwa kununua mitihani.
“Mfano hai kwa wilaya hii tulikuwa tukiwaona wazazi wa wanafunzi
waliokuwa wakitaka kufanya mitihani wakipanga foleni kwenye migahawa na
kila mmoja alikuwa akitozwa kuanzia sh 20,000, wakisubiri walimu ili
wapatiwe mitihani kwa ajili ya watoto wao.
“Utakuta mwanafunzi amefaulu darasa la saba kwenda kidato cha kwanza
lakini hajui kusoma wala kuandika, unajiuliza alifanya vipi mtihani
mpaka akafaulu, kumbe alipata fursa ya kufanyiwa mtihani na kupewa
majibu,” alifafanua Bayo.
No comments:
Post a Comment