Kama kuna suala nyeti kwa taifa ambalo
Serikali bado inalifanyia mzaha, basi suala hilo ni namna uraia
unavyotolewa kiholela kwa wageni pasipo kuwapo mfumo stahiki wa
kusimamia mchakato huo. Kwa muda mrefu sasa, Serikali imekuwa ikiliona
suala hilo la uraia kama jambo jepesi tofauti na nchi nyingi duniani
ambazo huliona kama msingi wa usalama na kitovu cha maendeleo ya nchi
hizo.
Hapa tunajaribu kuonyesha jinsi sera ya Serikali kuhusu uraia na uhamiaji inavyoendelea kututesa, ingawa inawezekana kabisa kwamba lipo kundi la watu linaloweza kuwa limefaidika na kuneemeka kutokana na udhaifu wa sera hiyo inayotoa mianya tele kwa vitendo vya rushwa na ufisadi. Hoja hapa ni kwamba Serikali inaendelea kutoa uraia kwa wahamiaji wengi wasiokuwa na sifa za kupata uraia wa Tanzania.
Wiki iliyopita, Serikali kama kawaida yake ilitoa tangazo tunaloweza kuliita la kisanii katika baadhi ya magazeti kuhusu watu walioomba uraia wa Tanzania. Pamoja na tangazo hilo kuficha mambo mengi muhimu kuhusu watu hao, linamtaka Mtanzania yeyote anayepinga watu hao kupewa uraia amwandikie Waziri wa Mambo ya Ndani na kutoa sababu kwa nini wasipewe uraia.
Hiki ni nini kama siyo kichekesho cha mwaka? Inawezekanaje tangazo lisilokuwa na kichwa wala miguu, kwa maana ya kuwa na taarifa muhimu za waombaji wa uraia lililotoka mara moja tu, tena katika gazeti moja au mawili liwawezeshe Watanzania wengi kuwafahamu watu hao na kuitaarifu Serikali? Je, watawezaje kuwasiliana na Serikali wakati tangazo hilo halionyeshi anuani au simu ya waziri au wizara husika? Serikali kweli ina dhamira ya kuwahusisha wananchi katika mchakato huo wa kuwapa au kutowapa uraia watu hao?
Tatizo hapa ni kwamba suala la kutoa uraia limepewa usiri mkubwa. Ndiyo maana kwa makusudi taarifa inayotolewa na Serikali kuhusu watu hao inakuwa nusunusu ili kuwachanganya wananchi wenye pingamizi wasijue pa kuanzia. Na ndiyo maana hata baada ya zoezi hilo Serikali haitoi taarifa kwa umma kuhusu waliopata na walionyimwa uraia.
Zoezi la kutoa uraia hufanywa kwa tahadhari kubwa katika nchi nyingi duniani. Kwanza, mwombaji lazima atume maombi akiwa nchini mwake. Hapa tunashuhudia watu wakiingia nchini ovyo na baadaye kuomba uraia.
Pili, kuna vigezo vinavyoangaliwa, ikiwa ni pamoja na umuhimu wa elimu na taaluma yake kwa nchi anayoomba uraia; au umri na uwezo wake wa kiuchumi wa kumwezesha kujitegemea; au sababu za kibinadamu kama kukimbia vita, mateso, na kadhalika.
Uzoefu umeonyesha kwamba nchi yetu inatoa uraia kwa watu wazima na tegemezi ambao hawawezi kuwa na manufaa yoyote kwa nchi yetu. Tunatoa uraia kwa watu wanaogeuka wachuuzi na kupigana vikumbo mitaani na vijana wetu wasio na ajira. Hii inatokana na baadhi ya ndugu zao ambao tayari wana uraia wa Tanzania (ambao waliupata kinamna?) kutoa rushwa na kuwawezesha kupewa uraia.
Ndiyo maana Tanzania imekuwa kama nchi isiyo na mwenyewe ambayo inajulikana kwa jina la mitaani kama Shamba la Bibi. Tumegundua gesi na hivi punde tutagundua mafuta.
Uraia sasa utazidi kutolewa kama njugu, kwani wageni watamiminika ili kufaidi nishati hizo. Tusipokuwa makini tutaiuza nchi yetu.
No comments:
Post a Comment