SHAHIDI wa kwanza upande wa utetezi katika kesi inayowakabili
watu 10 wanaodaiwa kufanya vurugu katika mkutano wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Shabani Limu, ameiambia mahakama
kuwa Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba ndiye aliyekodi
kikundi hicho ili kifanye fujo.
Mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida Tersophia Tesha,
shahidi huyo alidai kuwa walipata taarifa kuwa Mwigulu ndiye aliyekodi
kikundi hicho ambacho baadhi ya washtakiwa ni wakazi wa jijini Dar es
Salaam ili kifanye fujo na mkutano wa CHADEMA usifanyike.
Limu ambaye pia ni Kaimu Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Singida, alifichua
siri hiyo wakati akitoa ushahidi katika kesi ya kufanya fujo na kupiga
watu mawe kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha
Ndago Jimbo la Iramba Magharibi.
Washtakiwa 10 wanakabiliwa na mashtaka ya kufanya vurugu na kupiga watu mawe kwenye mkutano wa hadhara wa CHADEMA.
Katika ushahidi wake, Limu alidai kuwa alikuwa mratibu wa mkutano huo
na kwamba hata kabla ya kuanza walijua kuna kikundi cha watu
waliokodiwa kwa ajili ya kuuvuruga.
Alidai kuwa baada ya Ofisa Sera na Utafiti wa CHADEMA Makao Makuu,
Mwita Waitara kusema kuwa Mwigulu anatumia jina lisilo lake na kwamba
ni mwogo ndipo vurugu zilianza kwa watu kupigwa mawe.
Aliongeza kuwa meza kuu walikoketi viongozi wa CHADEMA Taifa yaani
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, mshauri wa chama, Dk. Kitila Mkumbo
pamoja na Waitara haikudhurika na fujo hizo wala hakuna mali
iliyoharibiwa.
Baada ya maelezo hayo ya shahidi huyo, Mwendesha Mashtaka Mkaguzi wa
Polisi, Shukran Magafu alimuuliza maswali kama ifuatavyo:
Swali: Je, ni hawa washtakiwa waliopo mahakamani ndio waliokuwa wanapiga watu mawe?
Jibu: Sina hakika kwa kuwa nilificha uso wangu kwa kiti ili nisipigwe mawe.
Swali: Je, washtakiwa uliishawaona kabla ya siku ya tukio au ni wakazi wa Mkoa wa Singida?
Jibu: Sijawahi kuwaona na kwa ujumla washtakiwa hawa sio wakazi wa Mkoa wa Singida.
Naye mshitakiwa Mohamed Abdala alipata fursa ya kumhoji shahidi huyo
kama ndiye anatunza rekodi ya wakazi wa Singida hadi awafahamu wakazi
wote wa mkoa huo.
Washtakiwa waliokuwepo mahakamani hapo ni Abdala Mbwana, Laizimu
Njama, Ludovic Muganizi, Justin Sanga, Salum Ali na Mohamed Abdallah
wote ni wakazi wa jijini Dar es Salaam.
Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa tena Mei 6 mwaka huu na washtakiwa wote wako nje kwa dhamana.
Hata hivyo, Magafu aliieleza mahakama kuwa washtakiwa wengine,
Shabani Hamisi na Daniel Wambura ambao ni wakazi wa Kijiji cha Ndago
waliisharuka dhamana mapema kesi hiyo ilipoanza.
Washtakiwa hao wote kwa pamoja wanashtakiwa kwa kutenda kosa hilo
Julai 14 mwaka jana, saa 8:30 mchana kwenye mkutano wa hadhara wa
CHADEMA uliofanyika katika Kijiji cha Ndago na hivyo kusababisha
kuvunjika amani na utulivu kwa muda.
CHANZO TANZANIA DAIMA
CHANZO TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment