BANANA Zoro ameamua kurudi katika jukwaa la muziki wa kizazi kipya ili kuvaana na ushindani uliopo.
Mwanamuziki hiyo ameamua hivyo baada ya kukaa nje
kwa muda wa miaka mitano akiwa anafanya shughuli za bendi yake ya B-Band
inayotumbuiza kwa nyimbo mchanganyiko kwa mikataba hotelini.
"Nimefanya kwenye bendi kwa muda mrefu hivyo basi
sasa nimeamua kurudi kwenye huu muziki wa ushindani sokoni, kwani sioni
kipya kwangu ambacho kitanifanya nishindwe kufanya vizuri," anasema.
"Ninajua kuwa kuna wasanii wengi waliochipukia ambao kazi zao zinabamba lakini nitabanana nao. Simaanishi kwamba nitaacha kupiga bendi hapana, nitaendelea kama kawaida ila nataka niwape mashabiki wangu ladha tofauti baada ya kupokea maombi mengi kutoka kwao ya kunitaka nirudi kwenye ushindani sokoni."
Banana anasema maisha ya umaarufu ni presha kwani muda wote mashabiki wanatarajia vitu vizuri kutoka kwako na kwamba wewe ndiye unayeonekana kuwa kioo cha jamii tofauti ilivyo sasa.
"Wasanii wanatakiwa wabadilike na waende na wakati siyo kulumbana, kugombana, kutupiana vijembe kupitia mitandao ya kijamii ambayo kwa namna moja au nyingine huchochea suala fulani kuwa kubwa tofauti na lilivyo," anaongeza.
"Unajua suala hili linatokana na baadhi ya wasanii kutokuwa na watu wa karibu ambao watawapa ushauri wa kufanya jambo fulani la maendeleo.
"Kwa takwimu nilizonazo, asilimia 70 ya wasanii
wanahojiwa na kutaja mali zao ni waongo wanashindwa kusema ukweli wa
mambo, wengi wao wanaosema wakianza kushuka kwenye 'gemu' siri zao
zinafichuka kuwa mali hizo si zao."
Anasema muziki huo umekuwa wa gharama na kama huna fedha basi kurudi kwenye chati kama awali itakuwa ngumu, kwani asilimia 60 ya wasanii wameungana na madj au wamiliki wa vyombo vya habari ili kujipandisha chati.
"Hapo ndipo utaona ugumu uliokuwapo kwani ukipeleka wimbo wako uchezwe redioni mmiliki au dj anajiuliza acheze wimbo upi? Wa msanii wake au wako," anasema.
"Anajiuliza hivyo kwani akicheza wimbo huo wako
basi msanii wake hatawika kwenye soko, anaamua kupiga wimbo wa msanii
wake kwanza, kwa hali kama hii siwezi kushangaa kwa msanii waliotamba
hapo awali kurudi kwao kwenye 'gemu' kukawa kazi," anasema Banana.
Banana anasema kuwa ana albamu nyingi ila ile ya
kwanza ambayo ilibeba wimbo 'Mama Yangu' hataisahau kwani ndiyo
iliyomtambulisha rasmi kwenye anga za muziki kwa kufanya vizuri kwenye
soko.
No comments:
Post a Comment