WAKATI kocha wa Bayern Munich, Jupp Heynckes, akipania kufanya
mauaji dhidi ya Borussia Dortmund kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa
Ulaya leo Jumamosi, mpinzani wake Jurgen Klopp bado anashangazwa na
jinsi walivyofanya kufuru na kutua kwenye fainali hiyo itakayochezwa
kwenye Uwanja wa Wembley.
Borussia Dortmund ilitua fainali baada ya kupangwa
kwenye kundi la kifo dhidi ya Real Madrid, Manchester City na Ajax
Amsterdam na baadaye ikawatoa Shakhtar Donetsk, Malaga na Real Madrid
lakini Klopp bado anashangaa haelewi nini kimetokea.
"Bado ninashangazwa na kiwango hicho. Kama tumefanya vizuri kwenye mechi hizo, tutawika hata kwenye fainali, jambo la msingi ni kuona kama tunaweza kucheza mechi ya kawaida," alisema.
Lakini wakati kocha huyo akishangaa na kuichukulia
mechi hiyo kuwa ni ya kawaida, mpinzani wake Heynckes amesema hawezi
kukubali kufika fainali mara tatu na kutoka mikono mitupu. Bayern Munich
ilifika fainali miaka ya 2010 na 2012 lakini haikuambulia kitu.
Bayern Munich imefika fainali ya msimu huu baada
ya kuziachia maumivu Valencia, BATE Borisov, Lille, Arsenal, Juventus na
Barcelona ambayo waliichapa jumla ya mabao 7-0 kwenye mechi mbili za
nusu fainali.
Huenda B.Dortmund ikawa na wakati mgumu kidogo kwa kuwa kiungo, Mario Goetze, ameumia misuli na tayari amesajiliwa na Bayern Munich kwa pauni 37 milioni.
Lakini nyota wa Poland, Robert Lewandowski, ambaye
aliichinja Real Madrid ataongoza mashambulizi. Kipa Roman Weidenfeller
amejaribu kufuta tetesi kuwa Goetze ni tatizo na ameongeza kuwa waliwahi
kuitandika Bayern Munich mabao 5-2 wakati mchezaji huyo akiwa hayupo
uwanjani.
Mechi hiyo itakuwa ya 101 kwa klabu hizo zilizokutana mara saba kwenye misimu miwili.
Kocha Heynckes alisema: "Timu zote zinafahamiana, lakini nadhani tuna nafasi kubwa."
Kama Heynckes akishinda atakuwa kocha wa nne
kupata vikombe vya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye nchi mbili tofauti.
Mara ya mwisho alipata ushindi mwaka 1998 akiwa na Real Madrid.
Nayo Dortmund inaamini inaweza kurudia mafanikio
ya mwaka 1997 ambapo, Lars Ricken, alitokea benchi na kufunga bao
lililofanya matokeo kuwa magoli 3-1 dhidi ya Juventus kwenye Uwanja wa
Olympiastadion.
Kikosi cha Juergen Klopp kina uwezo mkubwa wa kushambulia kwa kushitukiza na huenda hiyo ikawa ngao yao.
No comments:
Post a Comment