Habari hii na Tanzania Daima.
HATIMA ya dhamana ya Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilfred Lwakatare na Ludovick
Joseph, inatarajia kujulikana leo watakapopandishwa katika mahakama ya
Kisutu.
Wakati watuhumiwa hao waliofutiwa makosa ya ugaidi wakipandishwa
kizimbani leo, Tanzania Daima, imedokezwa kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM)
kinafanya mbinu za kukwamisha dhamana hiyo.
Chanzo cha Tanzania Daima, kimedokeza kuwa lengo la CCM kutia mkono
kwenye kesi hiyo ni kutaka kumnusuru Naibu Katibu Mkuu wake, Mwigulu
Nchemba, aliyesema anao ushahidi wa ugaidi na yuko tayari kuutoa popote.
Wakati Mwigulu akijinasibu kuwa tayari kutoa ushahidi wa ugaidi wa
Lwakatare, Mahakama Kuu iliwafutia mashtaka ya Ugaidi Lwakatare na
Ludovick.
Taarifa za uhakika zilizoifikia Tanzania Daima, zinabainisha kuwa
kabla ya mkutano wa siku mbili wa Rais, Katibu Mkuu wa CCM na wabunge
wa chama hicho uliofanyika Dodoma wiki iliyopita, Kamati Kuu ilikutana
na kujadili masuala mbalimbali likiwemo la Lwakatare.
Inadaiwa suala la kesi ya Lwakatare lilionekana kuwakera baadhi ya
wajumbe walioweka wazi kuwa badala ya kuiumiza CHADEMA imekuwa tofauti
na kumuweka katika mazingira mabaya Nchemba na CCM.
Chanzo chetu kinathibitisha kuwa katika kikao cha Kamati Kuu
kilichoketi Dodoma baada ya Rais kukutana na wabunge wa CCM tarehe 18 na
19 mwezi huu, Mwigulu Nchemba aliwalalamikia wajumbe kwa kumtelekeza
kuhusu suala la kesi ya Lwakatare.
“Mwigulu alisimama mara kwa mara kuomba kwa nini suala hilo ameachiwa
yeye binafsi limwangamize wakati ni suala la chama, na kadiri
linavyomwathiri yeye ndivyo linavyokiathiri chama, hivyo mwisho aibu
itakuwa ya wote,” alisema mtoa habari wetu.
Inasadikika katika kikao hicho ndipo lilitolewa shinikizo la kumtaka
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Eliezer Feleshi, akate rufaa haraka dhidi
ya uamuzi wa Mahakama Kuu kumzuia Lwakatare kupata dhamana.
Tanzania Daima, iliwahi kudokezwa kuwa Mwigulu ndiye aliyepanga namna
ya kupata mkanda wa video unaodaiwa kumwonyesha Lwakatare na Ludovic
wakipanga kumdhuru Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi Denis Msacky.
Mei 8 mwaka huu, Jaji Lawrence Kaduri wa Mahakama Kuu alikubaliana
na hoja za mawakili wa Lwakatare kuwa mashtaka ya ugaidi hayana maelezo
ya kutosha kuonyesha kuwa ni ya ugaidi akisema yalipaswa yawe na maelezo
yanayoelezea uhalisia wa ugaidi.
Hata hivyo, mahakama hiyo ilitupilia mbali maombi ya mawakili wa
watuhumiwa hao kupinga uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wa
kuwafutia kesi na kisha kuwakamata na kuwafungulia tena kesi yenye
mashtaka hayo hayo kwenye Mahakama ya Kisutu, Machi 20, mwaka huu.
Mei 13, mwaka huu, katika Mahakama ya Kisutu jopo la Mawakili wa
Lwakatare waliiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, impatie dhamana,
Lwakatare baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kumfutia,
mashtaka ya ugaidi yaliyokuwa yakimkabili yeye na mwenzake Joseph
Ludovick Rwezaura, ambayo hayana dhamana.
Mmoja wa mawakili hao, Peter Kibatala, aliliambia gazeti hili kuwa
walikuwa wamejiandaa kikamilifu kuhakikisha kuwa wangeweza kumtoa kwa
dhamana kwa kuwa walikuwa tayari wamekamilisha masharti ya dhamana.
Hata hivyo, jitihada zao ziligonga mwamba kufuatia kitendo cha hakimu
anayesikiliza kesi hiyo, Aloyce Katemana, kutokuwapo mahakamani na hivyo
kusababisha kesi hiyo kuahirishwa hadi leo ambapo mawakili na wafuasi
wa chama hicho wanatarajia Lwakatare apate dhamana.
Tanzania Daima ilimtafuta Naibu Katibu Mkuu huyo kuzungumzia suala
hili bila mafanikio kwani simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikani muda
wote.
No comments:
Post a Comment