HATIMAYE wafanyabiashara ndogondogo (Wamachinga) wamekubali
kufanya biashara katika eneo la Mlandege walikohamishiwa na Halmashauri
ya Manispaa ya Iringa kutoka eneo la Mashine Tatu.
Wiki iliyopita Wamachinga hao walifanya vurugu kubwa kupinga
kuondolewa katika eneo la Mashine Tatu walilodai lina wateja wengi
zaidi.
Vurugu hizo zilisababisha mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter
Msingwa, na Wamachinga 70 kushtakiwa kwa kuharibu mali na uchochezi.
Baadhi ya Wamachinga waliozungumza na Tanzania Daima, walisema
wameamua kuondoka katika eneo la Mashine Tatu baada ya kubaini
hawatoweza kuendeleza mivutano na vyombo vya dola vinavyowazuia
wasifanye biashara zao.
Walibainisha kuwa vurugu zilizotokea wiki iliyopita zilichangiwa na
baadhi ya watu ambao si wafanyabiasahara ndogondogo bali waliutumia
mwanya huo kutimiza mahitaji yao.
Wakati huohuo, jeshi la polisi mkoani Iringa juzi na jana
lilizidisha ulinzi kwenye maeneo mbalimbali pamoja na kuwakamata baadhi
ya watu waliokuwa wakitoa kauli za kichochezi katika vijiwe mbali
mbali.
Huku askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kwa mara ya kwanza
usiku wa kuamkia leo walionekana wakiweka ulinzi mkali katika maeneo
mbalimbali ya mji likiwemo eneo la soko la Kihesa, Mlandege, Mashine
Tatu na maeneo mengine.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, amewapongeza
Wamachinga kwa kurejea eneo la Mlandege walilopangiwa na uongozi wa
manispaa ya Iringa.
No comments:
Post a Comment