MADAKTARI Bingwa wanne kati ya 20 waliopelekwa nje ya nchi kwa
nyakati tofauti kujifunza zaidi kuhusu upasuaji na utaalam wa mifupa
wamerejea.
Kurejea kwa madaktari hao kulibainishwa jijini Dar es Salaam jana na
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Seif Rashid wakati akifungua
mafunzo ya upasuaji kwa madaktari bingwa 80 kutoka nchi mbalimbali
Afrika.
Mafunzo hayo yanafanyika kwenye Kitengo cha Mifupa cha Hospitali ya
Taifa Muhimbili (MOI) chini ya udhamini wa taasisi za Sign Fructure Care
International, Chuo Kikuu cha Saint Francisco,
AO Foundation zote za
Marekani wakishirikiana na uongozi wa MOI.
“Serikali inalielewa tatizo la ukosefu wa wataalamu bingwa wa upasuaji
na mifupa ndiyo maana tuliwapeleka 20 nje ya nchi kujiendeleza sasa
wanne kati yao wamesharudi.
“…Lakini mchakato wa kuwaandaa wataalamu hawa ni mrefu kidogo, kwa
sababu lazima wamalize masomo yao ya kawaida ya udaktari kabla ya kuwa
wataalamu mabingwa,” alisema.
Hata hivyo, Naibu Waziri huyo alielezea juhudi za serikali kuzitafutia
ufumbuzi changamoto zinazoikabili MOI na hospitali nyingine ikiwemo
msongamano wa wagonjwa kutokana na ongezeko la ajali nchini.
Alisema sababu ya serikali kujenga jengo la kisasa jirani na MOI
linalotarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu, litapunguza msongamano wa
wagonjwa wodini kwa vile litakuwa na uwezo wa kuwahudumia wagonjwa wengi
kwa wakati mmoja.
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Profesa Lawrence Museru, alisema mafunzo
hayo yatawasaidia madaktari wake kwa maelezo kwamba kila kukicha fani ya
upasuaji inaibuka na mambo mapya.
No comments:
Post a Comment