KESI iliyofunguliwa mkoani Pwani dhidi ya Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), imeonekana kuliweka pabaya shirikisho hilo, ambalo hivi
sasa linahaha ifutwe.
TFF imeburuzwa mahakamani mjini Kibaha na mdau wa soka, anayejulikana
kama Babu Adam ambaye alifungua kesi Mei 30 mwaka huu, na kusimamiwa na
Daniel Ngasa wakitaka haki dhidi ya Kiluvya United, iliyopokwa ubingwa
wa mkoa wa Pwani.
Kamati hiyo, iliamua kuivua ubingwa Kiluvya United, baada ya kupokea
malalamiko kutoka timu ya Al Etihad ya Mafia, ambayo ilikuwa mshindi wa
pili.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu
Katibu Mkuu wa TFF, Sunday Kayuni, alisema wamekitaka Chama cha Soka
Mkoa wa Pwani (Corefa), kifute kesi hiyo kwa manufaa ya soka la
Tanzania.
Kayuni ambaye pia ni Mkutugenzi wa Ufundi wa Shirikisho hilo, alisema,
tayari amekiandikia barua chama hicho, kukiagiza kishirikiane na mdau
huyo kufuta kesi hiyo kabla ya saa 11 jioni ya jana ili kuondoa
uvunjwaji na ukiukwaji wa kanuni na taratibu za katiba ya Corefa na TFF.
Alisema kuwa ibara ya 13 kipengele cha 14 katika Katiba ya Corefa,
hakiruhusu kupeleka suala lolote la soka mahakamani kama ilivyo katika
Katiba ya TFF, jambo ambalo kama Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa),
litabaini kuwepo kwa hali hiyo, Tanzania inaweza kufungiwa.
“Kama mnavyofahamu, timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ iko safarini kwa ajili
ya mchezo wa kimataifa na Morocco, sasa siwezi kuingilia uhuru wa
mahakama, kwa kuwa kesi iko mahakamani, ila kupitia Corefa, kesi hii
ifutwe mara moja kwa kuwa Fifa wakisikia kuwa tumekwenda kinyume na
katiba, watairudisha timu yetu na haitashiriki mashindano yoyote,”
alisema Kayuni.
Alibainisha kuwa Corefa wanao wajibu kuhakikisha wanaweka mambo sawa
haraka iwezekanavyo, kabla hayajaathiri mfumo mzima wa TFF, kutokana na
katiba zenyewe kutoruhusu masuala ya soka kupelekwa mahakamani.
“Mimi mwenyewe ndiyo nilikwenda kuisikiliza kesi hiyo jana mjini
Kibaha, lakini siwezi kuizungumzia sana ila ikiwa Corefa hawatafuta kesi
hiyo leo, basi Kamati ya Ligi itakutana kesho ili kutoa msimamo wake,”
alisema Kayuni.
No comments:
Post a Comment