JESHI la Polisi mkoani Rukwa linamshikilia Mwalimu Ased Job
(31) kwa kumtorosha mwanafunzi wa kike mwenye umri wa miaka 17
kisha kuishi naye kinyumba kwa zaidi ya miezi miwili sasa.
Mwalimu huyo ambaye anafanya kazi katika Idara ya Elimu katika
Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga anatuhumiwa kuishi na mwanafunzi
huyo anayesoma kidato cha pili kama mkewe kwa kipindi hicho
chote.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Peter Ngusa, akithibitisha
kutokea kwa tukio hilo alisema lilitokea Februari mwaka huu baada ya
mtuhumiwa kumtorosha mwanafunzi huyo na kumpeleka mkoani Mbeya kisha
kufanya taratibu za uhamisho kwa lengo la kumhamishia mkoani Mbeya ili
akaishi naye huko.
“Baada ya kukamilisha uhamisho huo mwanafunzi huyo alihamia mkoani
Mbeya kisha akaanza kuishi na mwalimu huyo kinyumba hadi mwisho
mwa Mei mwaka huu alipomrejesha mjini Sumbawanga na kuendelea
kuishi naye kinyumba kisha baadaye kukamatwa,” alisema.
Kwa mujibu wa Ngusa kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kunatokana na
taarifa za siri za wasamaria wema na kwamba anatarajiwa kufikishwa
mahakamani muda wowote mara baada ya ya upelelezi wa awali dhidi
ya shauri lake kukamilika.
Wakati huohuo polisi mkoani hapa inamshikilia mkazi wa
kitongoji cha Sumbawanga Asilia mjini hapa, Situati Shaban (23), kwa
madai ya kujifanya mtumishi wa serikali.
Kwa mujibu wa Ngasa mtuhumiwa huyo alitiwa nguvuni Mei 15 , mkwa
huu, saa tano asubuhi eneo la Bomani mjini hapa akijitambulisha
kuwa ni Hakimu wa Wilaya ya Nkasi.
Inadaiwa kuwa mshtakiwa kwa kushirikiana na mwenzake, Thomas Charles
(23), mkazi wa kitongoji cha Chanji, walishafanikiwa kutapeli sh
200,000 kutoka kwa Edson Noah (27) kwa ahadi ya kumpatia kazi ya
udereva wa gari la hakimu huyo ‘feki’.
“Baada ya kutoa kiasi hicho cha fedha kijana huyo alisubiri ili
aitwe kukabidhiwa gari hilo lakini siku kadhaa zilipita bila
kuitwa na badala yake alipoulizia alitakiwa kuongeza kiasi kingine
cha fedha ndipo alipostuka na kutoa taarifa polisi ambapo mtego
uliandaliwa na hatimaye kuwanasa watuhumiwa hao.
No comments:
Post a Comment