SERIKALI imeonya kuwa haitaruhusu watu wachache wakwamishe juhudi za
Serikali za kuunganisha nchi na mtandao wa barabara za lami.
Rais Jakaya Kikwete, alisema hayo jana katika eneo la Omugakorongo Kata
ya Ndama, wilayani Karagwe, wakati akiweka jiwe la msingi katika barabara ya
Kyaka –Bugene yenye urefu wa kilometa 59.1, inayojengwa kwa kiwango cha lami.
Rais Jakaya Kikwete akisimikwa kuwa Chifu wa Wahaya na kukabidhiwa mgolole na silaha za jadi za Wahaya katika sherehe ya kuzindua Wilaya mpya ya Kyerwa mkoani Kagera mwishoni mwa wiki. (Picha na Ikulu).
Alitoa kauli hiyo baada ya Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, kumuomba
amuunge mkono wakati wa kupambana na wananchi wanne, waliokataa kupokea fidia
na kubomoa nyumba zao, ili kupisha ujenzi wa barabara hiyo.
Dk Magufuli alisema watu hao, akiwemo mzee marufu wa Wilaya ya Karagwe,
Nehemia Kazimoto, wanataka fidia zaidi, la sivyo nyumba zao hazibomolewi au
watakwenda mahakamani.
Alisema wananchi 400 waliokumbwa na athari za kubomolewa nyumba kupisha
ujenzi wa barabra hiyo, wamelipwa fidia Sh bilioni 2.8 kwa mujibu wa sheria,
isipokuwa wananchi wanne tu akiwemo Kazimoto, ambao wamegoma kupokea fidia.
“Hata wakienda mahakamani, sisi hatutaingilia Mahakama, bali barabara
itaendelea kujengwa ikipitia katika maeneo yaliyoainishwa,” alisema Dk
Magufuli.
Akitoa mfano wa mzee huyo aliyewahi kuwa kiongozi katika vyama vya
wafanyakazi nchini, Dk Magufuli alisema amegoma kupokea fidia yake ya Sh
milioni 101, ambazo zilitolewa na Serikali huku akidai kuwa hazitoshi na wala
hatokubali nyumba yake ibomolewe kupisha barabara.
Kauli ya Rais
Akijibu maombi hayo, Rais Kikwete alimtaka Waziri Magufuli aendelee na
kasi ya kutekeleza mipango yake ya ujenzi wa barabara ya Kyaka Bugene, ili
ikamilike kwa wakati, ingawa kuna changamoto zinazokabili mradi huo kutoka kwa
baadhi ya wananchi ambao si wapenda maendeleo.
“Hatutaruhusu watu wachache wazime na kukwamisha maendeleo ya Watanzania
walio wengi, Waziri nimekusikia, endelea na mipango na kazi yako ya kujenga
barabara hii, ili Wanakagera na Watanzania, waendelee kunufaika na matunda ya
Serikali…tena hii ni ahadi yangu niliyoitoa wakati naomba kura mwaka 2005, pia
ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2010,”alisema Rais Kikwete.
Alisema lengo la ujenzi wa barabara hizo, ni kuhakikisha nchi
inaunganishwa kwa mtandao wa lami, kwani siku za nyuma wananchi wa Mkoa wa
Kagera waliteseka kwa kusafiri umbali mrefu, kwenda Dar es Salaam.
Wakati huo wananchi hao walilazimika kupita Uganda na Kenya kwa siku
tatu mpaka tano ili kufika Dar es Salaam, lakini sasa wanauwezo wa kusafiri kwa
siku moja tu kutokana na barabara kutengenezwa na kupitika kwa urahisi.
Mafanikio
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, anatarajia ifikapo 2015 kilometa 18,000 za
mtandao wa barabara wa Tanzania nzima zitakuwa tayari na kama itashindikana,
basi zitabaki kilometa zisizozidi 2,000, ambazo zitakuwa hazijakamika lakini
zitakuwa zikiendelea na ujenzi kwa hatua ya mwisho.
Naye Dk Magufuli, alisema wakati wa Uhuru 1961, nchi ilikuwa na mtandao
wa barabara za lami za urefu wa kilometa 1,350, lakini katika muda wa Serikali
ya Awamu ya Nne tu, chini ya uongozi wa Rais Kikwete, zimejengwa kilometa
11,154 za mtandao wa barabara kwa kiwango cha lami.
Akitoa historia ya ujenzi barabara ya Kyaka–Bugene, Dk Magufuli alisema
mradi huo ulianza 2009 na mpaka kukamilika, katika muda wa miezi 27, utagharimu
Sh bilioni 64.9.
Mradi huo kwa mujibu wa Dk Magufuli, unaendelea vizuri ingawa ulikumbwa
na changamoto mbalimbali, ikiwemo ya makandarasi wasimamizi wa mwanzo, Kampuni
ya Sai kutoka nchini India kwa kushirikiana na Kampuni ya Data ya Tanzania,
kufukuzwa kazi baada ya muda mfupi tangu kuanza mradi.
Alisema kuwa makandarasi hao walifukuzwa kazi, baada ya kuboronga na
kushindwa kufanya kazi kama mkataba unavyoelekeza, wakati tayari walikuwa
wamelipwa zaidi ya Sh bilioni moja. Kwa sasa mradi huo unasimamiwa na kikosi
cha wataalamu saba kutoka Wakala wa Barabara (Tanroads) Makao Makuu.
Alionya kuwa Wizara yake haitosita kuwachukulia hatu ikiwemo kuwafukuza
kazi makandarasi watakaokiuka utaratibu wa kazi, kwani Tanzania sio nchi ya
watu kuja kuchota fedha.
Naye Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Makao Makuu, Alon Mfugale, alisema mradi
huo wa barabara ya Kyaka –Bugene, unaojengwa na Kampuni ya China Chico kutoka
nchini China, umefikia asilimia 38 ya mradi wote mpaka sasa na unagharimiwa na
Serikali kwa asilimia 100.
VIA HABARI LEO
No comments:
Post a Comment