Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) kimepinga muswada wa Sheria ya kura ya maoni mbele
ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria, Katiba na Utawala kwa madai
kuwa utakwenda kinyume na katiba ya sasa.
Chama hicho kilikuwa cha mwisho jana kutoa
mapendekezo yake kati ya vyama vitano vilivyokuwapo ambavyo ni pamoja na
Demokrasia Makini, Tadea, Chaumma, NLD, NRA na AFP.
Huku akitaja kesi No. 45 ya mwaka 2009 kati ya
Mwanasheria Mkuu na Mchungaji Mtikila, mjumbe wa chama hicho, John Malya
alisema kuwa katiba ya sasa haitambui kura ya maoni hata kama inaruhusu
ushiriki wa wananchi.
Alisema ili kuwapo kwa sheria hiyo ni lazima kuibadilisha katiba ya sasa ili kuruhusu mchakato wake.
Hata hivyo mjumbe wa Katiba ya Kudumu ya Bunge ya
Sheria na Katiba na Utawala ambaye pia ni Mbunge wa Muhambwe, Felix
Mkosamali alisoma Katiba katika ibara ya 98 (1b) akisema kuwa inaruhusu
Bunge kutunga sheria yoyote inayoweza kubadili Katiba.
Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Pindi Chana
alisema kuwa Chadema wana kigeugeu kwani awali walikubali kuwepo kwa
kura ya maoni.
“Wakati tunapitisha muswada huu kifungu cha 6,
Chadema walileta maoni tena kwenye ukumbi huu… walikubali kuwapo kwa
kura ya maoni, lakini nashangaa leo wanapinga,” alisema Dk Chana.
Akijibu maoni hayo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika
alisema kuwa kifungu cha 98 cha katiba kimekuja mara ya pili kwani tangu
wakati wa kuanzisha Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba kilitumika
kuupinga.
“Mara ya kwanza watu walitumia kifungu cha 98 cha
Katiba wakisema hakuna haja ya kuandika Katiba Mpya. Unapozungumzia kuwa
Bunge linaweza kutunga sheria, ujiulize ni wabunge gani,’’ alisema.
No comments:
Post a Comment