MBUNGE wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), amelazwa katika
Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam akisumbuliwa na tatizo la
ugonjwa wa kiharusi (mild stroke).
Cheyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa UDP Taifa, alifikishwa hospitalini
hapo usiku wa Jumatatu wiki hii na hali yake inaendelea vizuri tofauti
na siku ya kwanza.
Akizungumza na gazeti hili hospitalini hapo, msemaji wa familia,
Maghende Cheyo, alisema hali ya kaka yake inaendelea kuimarika siku hadi
siku na kwamba wana uhakika wa kuruhusiwa mapema.
“Tunaamini ataruhusiwa mapema kinachomsumbua ni ‘mild stroke’ ila kwa
sasa yupo katika mazoezi na ni vema atakapomaliza apate muda wa
kupumzika,” alisema Maghende akiwa chumba namba 57 alicholazwa Cheyo.
Mmoja wa madaktari bingwa nchini aliyezungumza na gazeti hili
alifafanua kuhusu ugonjwa huo akisema kuna aina mbili za kiharusi na
kwamba zote zina madhara tofauti.
Alitaja aina hizo kuwa ni kiharusi kamili (full stroke) na kile cha kati (mild stroke).
Alisema madhara ya kiharusi kamili ni mgonjwa kupoteza fahamu, kupooza moja kwa moja au kufa papohapo.
Aidha, alisema madhara ya kiharusi cha kati ni mgonjwa kuongea kwa tabu, mdomo kwenda upande na upande wa uso kulegea.
Daktari huyo aliongeza kuwa aina hiyo ya pili inaweza kumchukua
mgonjwa muda wa mwezi mmoja hadi miwili kurejea katika hali ya unafuu.
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete juzi usiku alimtembelea na kumjulia hali Cheyo.
Rais Kikwete alizungumza kwa muda na Cheyo akimpa pole na kumtakia
apone haraka ili aweze kuendelea na shughuli zake za uwakilishi wa
wananchi wa Bariadi Mashariki.
No comments:
Post a Comment