HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbozi, mkoani Mbeya imepata hasara ya
mamilioni ya fedha kutokana na kukosa kumbukumbu za vyanzo vyake vya
mapato, zikiwamo nyumba inazomiliki kwa zaidi ya miaka 20 bila
kuwatambua wapangaji wake kisheria.
Nyumba hizo tatu ambazo ziko katikati ya mji wa Vwawa wilayani hapa
kwa sasa zinatumika kama nyumba za biashara ya kupangisha wageni ‘guest
house’, baa na ofisi, ambapo moja ni ofisi ya Ushirika wa Umoja wa
Wanawake na nyingine ni ya Tanganyika Farmers Association ( TFA).
Hoja ya upotevu huo wa mapato iliibuliwa na Diwani wa Ihanda, Joel
Kasebele na baadaye kuungwa mkono na madiwani wengine kwenye kikao cha
kawaida cha baraza la madiwani wa Halamshauri ya Wilaya ya Mbozi.
Diwani Kasebele alimuuliza Mkurugenzi Mtendaji wa halmshauri hiyo
ambaye ndiye katibu wa kikao hicho juu ya mustakabali wa nyumba hizo
zinazojulikana kwa majina ya TFA, Selfina na MDC (Mbozi District
Council) ambazo zinadaiwa kumilikiwa na halmashauri hiyo tangu mwanzoni
mwa miaka ya 1980 ulipoanzishwa mfumo wa serikali za mitaa.
Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Levison
Chilewa, alikiri kuwapo kwa nyumba hizo pamoja na nyingine zilizokuwa
zikimilikiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na baadaye kuiuzia
halmashauri hiyo.
Pia alikiri kuwapo kwa wapangaji, lakini haijulikani walikodishwa na nani na ni kwa kipindi gani (miaka mingapi) hadi sasa.
hata hivyo, alijitetea kuwa yeye na wataalamu wengi wa halmashauri
hiyo ni wageni, hivyo hawakukuta kumbukumbu zozote ofisini kutoka kwa
waliowarithi.
Kutokana na hali hiyo, aliliomba baraza hilo kumpatia muda
kulifuatilia jambo hilo na kuahidi kulitolea maelezo katika kikao
kijacho.
Habari na na Kenneth Ngelesi, Mbozi ,Tanzania daima.
No comments:
Post a Comment