MKAZI wa Mbagala, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, Rashidi
Mwinyimkuu, anadaiwa kutapeli watu fedha na vitu mbalimbali kwa
kujifanya ni Ofisa Usalama wa Taifa.
Mwinyimkuu anayedaiwa kuwa karibu na baadhi ya askari amekuwa akifanya
vitendo hivyo kwa muda mrefu sasa bila vyombo vya dola kumtia hatiani
huku taarifa zake zikidaiwa kufikishwa kwenye Kituo Kidogo cha Polisi
Charambe.
Wakizungumza kwa wakati tofauti na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam juzi, baadhi ya wakazi hao walisema watu kama hao wamekuwa
wakichafua heshima ya serikali.
Walisema Mwinyimkuu alifanikiwa katika baadhi ya vitendo vyake vya
utapeli kwa sababu alikuwa ana kitambulisho kilichokuwa kikimtambulisha
kuwa ni Ofisa Usalama wa Taifa.
Katika tukio la hivi karibuni, Mwinyimkuu alimtapeli Ibrahimu Kipande
sh 200,000, akidai kuwa angempatia kazi ya udereva kwenye moja ya Ofisi
za Uslama wa Taifa jijini Dar es Salaam.
“Tulianza kumtilia shaka kutokana na tabia yake ya kupenda kujifaragua
mbele za watu kwa kujitambulisha kila anapokutana na watu akisema mimi
ni Ofisa Usalama hata bila kuulizwa,” alisema Kipande.
Hata hvyo baada ya kushindwa kutekeleza ahadi yake, Kipande
alilifikisha suala hilo kwenye Kituo Kidogo cha Polisi Charambe ambako
mkuu wa kituo hicho alilimaliza kimya kimya, kwa mdai kulipwa fedha
zake.
Kwa upande wake Mwinyimkuu, alisema taarifa hizo hazina ukweli wowote.
“Sijafanya kazi ya Usalama wa Taifa na wala sijajifanya hivyo, mimi
watu wote huku kwetu wananijua kazi yangu kuwa ni mtumishi wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), hadi kupachikwa jina la Mwinyimkuu CCM,” alisema
Mwinyimkuu.
Mkuu wa Kituo hicho cha Polisi, Jonas, alisema anamfahamu mtu huyo
kama mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Chalambe, lakini hajafikishwa kwenye
kituo hicho kwa tuhuma hizo za utapeli.
No comments:
Post a Comment