SERIKALI imetangaza kuwapatia mikopo wanafunzi wa elimu ya juu
29,754 kati ya wanafunzi 31,647 katika mwaka wa masomo 2013/2014.
Mkurugenzi wa Habari, Elimu na Mawasiliano, Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Cosmas Mwaisobwa, alieleza hayo jijini Dar
es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu utaratibu wa
utoaji wa mikopo hiyo kwa wanafunzi wapya na wanaoendelea na elimu ya
juu.
Alisema uchambuzi wa maombi ya mikopo kwa mwaka huu wa masomo
umekamilika na kwamba lengo la serikali ni kuwawezesha wanafunzi wa
elimu ya juu kupata fedha kwa muda muafaka.
Alisema kuwa mchanganuo wa utuoaji wa mikopo hiyo ulizingatia vigezo na masharti ya uombaji mikopo na ruzuku.
Alisema idadi ya waombaji wapya waliotuma maombi yalikuwa 53,239,
waombaji wanaoendelea na masomo 43,032, waombaji waliokuwa na maombi
yenye matatizo ni 6,364.
“Wengine ni waombaji waliorekebisha matatizo kwenye maombi yao 3,151
na waombaji ambao hawakurekebisha matatizo kwenye maombi yao 3,213,”
alisema.
Akifafanua zaidi kuhusu mchanganuo huo alisema waombaji wapya 53,630 watakaosoma ndani na nje ya nchi wamepata mikopo hiyo.
Alisema maombi ya mikopo kwa wanafunzi wanaoendelea 61,692 ambao
wanasoma ndani na nje ya nchi wamepangiwa kupata mikopo hiyo.
Mkurugenzi huyo alisema bodi ya mikopo ya elimu ya juu inatarajia
kutoa mikopo ya sh bilioni 306 kwa ajili ya ukopeshaji wanafunzi wapya
na wanaoendelea na masomo.
Alisema mchakato wa upangaji wa mikopo unaendelea vizuri na kwamba hadi sasa umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.
“Matarajio ni kukamilisha mchakato huu kwa asilimia 100 ifikapo wiki
ya kwanza ya Oktoba kabla ya vyuo vya elimu ya juu kufunguliwa, kwa
mujibu wa Tume ya Vyuo Vikuu,” alisema.
Alieleza kuwa orodha kamili ya waombaji wapya waliopangiwa mikopo
inapatikana kwenye tovuti ya bodi hiyo www.heslb.go.tz ambapo mwombaji
anaweza kutafuta jina lake kwa kutumia namba ya mtihani ya kidato cha
nne.
Alisisitiza kuwa taratibu za kupeleka mikopo yao vyuoni zinaendelea na kwamba watalipwa baada ya kufanya usajili.
Aidha alisisitiza umuhimu wa kila mwombaji kuwa na akaunti ya benki kwa ajili ya kupitishia mikopo hiyo.
Aliongeza kusema kuwa waombaji waliofanikiwa kupangiwa mikopo
wanawajibika kurejesha mikopo hiyo baada ya kuhitimu masomo yao.
No comments:
Post a Comment