HALI bado tete nchini Kenya kufuatia tukio la magaidi kuteka
jengo la kibiashara la Westgate mwishoni mwa juma na kuwaua watu wapatao
62 hadi sasa, huku wengine zaidi ya 175 wakiwa wamejeruhiwa.
Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya, Joseph ole Lenku amesema idadi
kubwa ya mateka wameokolewa na jeshi baada ya kudhibiti sehemu kubwa ya
jengo hilo.
Jeshi hilo limefanikiwa kuwaokoa katika operesheni ya kuhakikisha
wanawakomboa mateka waliokuwa wakishikiliwa na wanamgambo hao wa kundi
la Al-Shabaab.
Ole Lenku aliongeza kuwa hadi jana wanajeshi wao walikuwa wamefanikiwa
kuwaua wapiganaji wawili wa kundi hilo na wengine baadhi kujeruhiwa.
Hivi sasa shughuli mbalimbali zimesimama kutokana na wananchi na
viongozi nchini humo kutazama kinachoendelea, huku misaada ya aina
mbalimbali ikiendelea kutolewa ikiwemo uchangiaji damu kwa ajili ya
kuokoa maisha ya majeruhi ambao wengine wamefanyiwa upasuaji.
Serikali za Tanzania, Rwanda, Uganda na Burundi zimelaani shambulio
hilo na kutoa pole kwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta pamoja na wananchi
wa taifa hilo ambao wamepoteza ndugu zao.
Jeshi lilikuwa limeshadhibiti
jengo hilo huku hali ya ufyatulianaji risasi ikiendelea kushuhudiwa
katika jengo hilo ambalo lina maduka zaidi ya 80.
Milio hiyo ilidumu kwa dakika tatu na kufuatiwa na moshi mkubwa juu ya
jengo hilo, huku kukiwa na taarifa za kutatanisha juu chanzo cha kuzuka
kwa moshi huo ingawa baadaye ilielezwa kwamba ulikuwa ni mkakati wa
jeshi kutaka kuwapumbaza maadui.
Jeshi halijaweka bayana kama watekaji hao 15 wanaodaiwa kuwa ndani ya
jengo hilo wameuawa au bado wako hai baada ya kuwazingira.
Rais Kenyatta amesema kuwa jeshi linajitahidi kuhakikisha kuwa linakabiliana vilivyo na wanamgambo hao.
Helikopta za polisi zimeonekana zikiendelea kuzunguka juu ya jengo hilo pamoja na ndege za kijeshi kuendelea kufanya doria.
Kauli ya Marekani
Rais Barack Obama wa Marekani amempigia simu Rais Kenyatta na kumpa pole kwa niaba ya Wamarekani kutokana na shambulizi hilo.
Taarifa ya Ikulu ya Marekani imeeleza kuwa Obama ameahidi kumuunga
mkono Kenyatta katika jitihada za kuusambaratisha mtandao wa kundi hilo
la Al-Shabab.
Al- Shabaab imekiri kuhusika na shambulio hilo kwa nia ya kulipa
kisasi cha kupigwa na kuondolewa nchini Somalia ambako Kenya imetuma
jeshi lake tangu mwaka 2011.
Ruto arejea
Katika hatua nyingine majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa
Kivita (ICC), wameahirisha kesi inayomkabili makamu wa Rais wa Kenya,
William Ruto kwa wiki moja ili kumpa muda kurejea nyumbani kushughulikia
hali ya kiusalama inayolikumba taifa hilo.
Ruto na Rais Kenyatta, wanakabiliwa na tuhuma za uhalifu dhidi ya
binadamu baada ya kudaiwa kuhusika na ghasia za kikabila baada ya
uchaguzi wa mwaka 2007/2008. Watu zaidi ya elfu moja waliuawa.
Akizungumzia kuhusu tukio hilo, jaji anayesimamia kesi yake, Chile
Eboe-Osuji alisema: “Mahakama inamruhusu Ruto kurejea nyumbani kwa muda
wa wiki moja ila kama ataongeza siku itambidi kuandika ombi jingine.”
No comments:
Post a Comment