MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Mukubu, Wilaya ya Ngara mkoani
Kagera, Silidion Kaiza (43), anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa
tuhuma za kukutwa na bangi gunia sita.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi alisema kuwa tukio
hilo lilitokea Septemba 17, mwaka huu, shuleni hapo katika kata na
kijiji cha Muganza majira ya saa tano asubuhi.
Alisema kuwa raia wema walitoa taarifa kituo cha polisi Rulenge
kwamba kuna mwalimu anajihusisha na biashara ya kuuza dawa za kulevya,
jambo walilohofia kuwa huenda akawaathiri wanafunzi wa shule hiyo kwani
anazihifadhi shuleni.
Kalangi alifafanua kuwa baada ya polisi kupata taarifa hiyo walifika
shuleni hapo na kumhoji mwalimu Kaiza, na alikiri kufanya biashara hiyo
kisha akawapeleka katika moja ya darasa ambalo alikuwa akitunza bangi
hiyo.
Kamanda alisema kuwa baada ya polisi kukamata bangi hiyo,
waliifikisha kituoni na kwamba mwalimu huyo anaendelea kuhojiwa kisha
atafikishwa mahakamani wakati wowote ili kujibu tuhuma hizo.
Aliwataka wananchi kuendelea kuwafichua wahalifu wanaojihusisha na
vitendo vya uuzaji wa dawa za kulevya ambavyo vimekuwa tishio kwa
taifa.
No comments:
Post a Comment