WAKATI hali ikiwa tete wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli Tanzania
na Zambia (TAZARA) wanaoendelea na mgomo wa kusotea malipo yao, suala
hilo jana lilitinga bungeni na kuibua tafrani kubwa.
Akizungumza Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli
(Trawu) Kanda ya Dar es Salaam, Theresia Mahagatila, alithibitisha
kuendelea kwa mgomo huo kutokana na uongozi wa TAZARA kuwadanganya
wafanyakazi.
Licha ya TAZARA kuahidi kulipa malimbikizo hayo ya mshahara ya miezi
minne ifikapo Agosti 29 mwaka huu, ahadi hiyo imeota mbawa na badala
yake imelipa mshahara wa mwezi wa tano pekee.
“Sisi tulifika ofisini tayari kwa kazi siku hiyo kama walivyotangaza
kwenye vyombo vya habari, cha kushangaza tumelipwa mshahara wa mwezi wa
tano tu na waliolipwa ni baadhi yetu,” alisema.
Makuu ya TAZARA jana na kukuta
wafanyakazi hao wakiwa kwenye makundi huku huduma zote zikiwa
zimesimama.
Wakati hali ikiwa hivyo TAZARA, mjini Dodoma, Bunge nusura zisimame
baada ya mbunge wa Viti Maalum, Suzan Kiwanga (CHADEMA), kutaka shughuli
zisitishwe ili lijadili kufukuzwa kazi kwa wafanyakazi hao.
Kiwanga alibainisha kuwa kufukuzwa kazi kwa wafanyakazi hao
kunawafanya baadhi ya wananchi hususan wa mikoa ya Kusini kujawa na hofu
ya reli hiyo kuhujumiwa na hivyo uchumi wa mikoa hiyo kutetereka.
Mbunge huyo mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na
majibu, aliomba mwongozo wa Spika kwa mujibu wa Kanuni za Bunge kifungu
cha 47 (1) na 48 inayolitaka Bunge kusitisha shughuli zake ili kujadili
jambo zito litakalowasilishwa na mbunge.
Kiwanga alibainisha kuwa kufukuzwa kazi kwa wafanyakazi hao kumemfanya
asipate usingizi na familia zaidi ya 9,000 zimeathirika.
Alisema kuwa alipigiwa simu nyingi na wananchi baada ya wafanyakazi 1,500 wa TAZARA kufukuzwa wakihofia uchumi wao kuporomoka.
“Ninaliomba Bunge liahirishe shughuli zake ili lijadili jambo la TAZARA kwa kuwa linagusa maslahi ya wananchi wengi.
“Hivi jamani tuwe wakweli tungefanyaje kama sisi wabunge tungekuwa
hatujalipwa mishahara yetu kwa miezi minne, tungekubali?” alihoji.
Kiwanga alibainisha kuwa anashangazwa na hatua zilizochuliwa na
menejimenti ya TAZARA (Tanzania) kuwafukuza kazi wafanyakazi wake wakati
wenzao wa Zambia waliwalipa wafanyakazi wao waliogoma kwa siku nne.
Mbunge huyo alihoji kwa nini serikali ya Tanzania ina kigugumizi cha
kuzungumzia jambo hilo au kutekeleza mahitaji ya wafanyakazi.
“Zambia waligoma kwa muda wa siku nne na walitimiziwa stahiki zao
lakini Tanzania hali imekuwa sivyo, inasuasua kwenye suala hilo
linaloweza kusababisha uchumi wa nchi kuporomoka kutokana na athari za
mgomo huu, kwa nini tumefikia hapa?” alisisitiza.
Baada ya Kiwanga kumaliza kuomba mwongozo huo, Naibu Spika Ndugai,
alimtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge),
William Lukuvi, kutoa ufafanuzi kuhusu sakata hilo.
Lukuvi alisema kuwa menejimenti ya TAZARA imefuta uamuzi wa kufukuzwa
kwa wafanyakazi hao na serikali itatoa taarifa bungeni kulingana na
nafasi ya Bunge.
No comments:
Post a Comment