MWENYEKITI Serikali ya Mtaa Ruguluni, Wilaya ya Kinondoni, Dar
es Salaam, Saidi Mahadula, amesema mtaa huo haujawahi kuwa na shule ya
msingi tangu ulipoanzishwa miaka 14 iliyopita.
Mahadula alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki kwenye mkutano wa
hadhara uliokuwa ukijadili maendeleo na kero za mtaa huo, uliofanyika
kwenye viwanja vya Dk. Halid, Makondeko.
Alisema kutokana na kukosekana kwa shule katika mtaa huo, watoto
hulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata shule, jambo ambalo wakati
mwingine ni hatari kutokana na baadhi yao kuwa na umri mdogo.
Aliyataja maeneo ambayo watoto hao wamekuwa wakifuata shule kuwa ni Mbezi Luis, Kibamba, Mpijimagohe na Mshikamano.
“Umefika wakati wa kuunganisha nguvu zetu na tushirikiane, ili kwa
pamoja tuweze kumaliza kero inayotukabili,” alisema Mahadula.
Ili kumaliza kero hiyo, wakazi hao kwa pamoja wamekubaliana kuanzisha
mchakato wa kujenga shule kwa kuanzisha kitu walichokiita ‘Dira ya
Maendeleo’.
Mahadula alisema lengo la dira hiyo ni kutafuta fedha kutoka manispaa
ya Kinondoni, Serikali Kuu, wafadhili wa ndani na nje ya nchi, kampuni
za simu, wadau mbalimbali na wakazi wa mtaa huo ili kufanikisha azma
hiyo.
No comments:
Post a Comment