KWA mara nyingine serikali imeendelea kuandama vyombo vya
habari viwili ilivyovifungia wiki iliyopita, magazeti ya Mwananchi na
Mtanzania.
Jana ilitishia kuchukua hatua kali dhidi ya gazeti la Rai (dada wa
Mtanzania) ikisema iko tayari kulifunga iwapo litaendelea kuchapishwa
katika siku tofauti na Alhamisi.
Kupitia kwa Mkurugenzi wa Habari (MAELEZO), Assah Mwambene, serikali
jana ilisema haitaki kuliona gazeti la Mwananchi mtandaoni kama ambavyo
hailitaki mitaani.
Mwambene alipiga marufuku magazeti hayo kuonekana popote, kwa njia yoyote, kabla hayajamaliza kifungo.
Mwambene alisema kuwa gazeti la Mwananchi baada ya kufungiwa
limeendelea kutoa habari zake kupitia tovuti ya gazeti lao kinyume cha
amri iliyotolewa na kwamba serikali imewaandikia kuwataka kuacha mara
moja la sivyo watalazimika kuchukua hatua kali zaidi.
“Kampuni ya New Habari 2006 baada ya kufungiwa moja ya magazeti yake,
imeanza kuchapisha gazeti la ‘Rai’ kila siku tangu Septemba 29,
mwaka huu bila ya kibali cha Msajili wa Magazeti,” alisema.
Hata hivyo, amri ya serikali ya kuzuia Rai kutoka kila siku hasa
baada ya Mtanzania kufungiwa siku nne zilizopita, imekumbana na
upinzani mkali kutoka kwa uongozi wa New Habari.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano kwa njia ya simu, Afisa
Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Hussein Bashe, alisema kuwa kauli ya
mkurugenzi wa MAELEZO inaonyesha bayana jinsi serikali ilivyokusudia
kuiangamiza kampuni yake.
Bashe alimshambulia Mwambene akidai kuwa huenda mkurugenzi huyo hajui
sheria za kuendesha makampuni au ana nia mbaya na tasnia ya habari
nchini kwa sababu Rai imesajiliwa na ina kibali cha kutolewa kila siku.
“Rai ni gazeti lililosajiliwa kutoka kila siku kwa kibali cha
serikali kilichotolewa na msajili wa magazeti Desemba 22, 1994 kwa
barua yenye kumb: IH/TN/283/12. Barua hiyo inasema: ‘Yah kuchapicha
gazeti la Rai kila siku’ na kutiwa saini na Dominica C. Haule, kwa
niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo).
Hata hivyo, Mwambene pamoja na kukiri barua hiyo, amedai kuwa
ilitolewa kwa kampuni ya Habari Corporation, na sio New Habari (2006)
Ltd, iliyonunua hisa za Habari Corporation.
Mwambene alisema kwa msingi huo, Rai haiwezi kuchapishwa kila siku kama anavyojaribu kusema Bashe katika utetezi wake.
Hata hivyo, Bashe alionekana kushangazwa na kauli ya mkurugenzi huyo
na kuhoji uelewa wake kuhusiana na sheria za biashara za kununua na
kuuza kampuni.
Alihoji ikiwa kampuni ilinunua hisa zote, itashindwaje au kuzuiwa
vipi kuendelea na uendeshaji wa shughuli ikiwa imenunua mali zote na
hivyo kuwa halali kuendeleza shughuli zinazotakiwa.
“Sisi tulichofanya ni kuitaarifu tu idara ya habari kwamba sasa
tutaendelea na kuchapa kila siku na tulifanya hivyo Jumamosi. Sasa
tunashangaa anaendelea tena kutusakama. Kuna nini hapa?” alihoji Bashe
kwa mshangao.
Mwambene alisema kuwa serikali imeyafungia magazeti ya hayo kwa
kuzingatia Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 na kanuni zake za mwaka
1977.
Alisema kuwa umma unapaswa kufahamu kuwa serikali haikukurupuka
kufungia magazeti hayo, baada ya kufuata taratibu zote za msingi
ikiwemo kuwasikiliza wahusika.
“Mwananchi limefungiwa kwa muda wiki mbili kuanzia Septemba 27,
mwaka huu, na Mtanzania limefungiwa kwa muda wa miezi mitatu au siku 90
kuanzia Septemba 27, mwaka huu,” alisema.
Aidha, serikali imelaumiwa kwa tamko lake la kulitaka gazeti la
Mwananchi kutowekwa mtandaoni mambo ambayo wachunguzi wanasema
yalipaswa kufanywa na mamlaka ya mawasiliano (TCRA), ambayo ndiyo yenye
mamlaka na mambo ya mitandao nchini kama kulikuwa na ukiukwaji
uliofanyika.
Wadau wanasema tofauti za kimajukumu kati ya Idara ya Habari na
Mamlaka ya Mawasiliano nchini ziko bayana ndio maana hata Rais Jakaya
Kikwete alitofautisha Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, huku
nyingine inayohusisha mambo ya mitandao ikiwa chini ya Mawasiliano
Sayansi na Teknolojia.
Hatua hiyo ya serikali imezidisha mpasuko mkubwa kati ya utawala na
vyombo vya habari, mashirika ya kiraia ndani na nje ya nchi.
Taasisi na mashirika hayo yamelaani hatua hiyo, huku yakiitaka
serikali kuacha kuzuia haki ya wananchi ya kujieleza na kupokea habari
na mengine yakienda mbali zaidi na kutuhumu kuwepo kwa hujuma ya
kuwanyima wananchi habari zinazoendelea kujiri katika mchakato wa Katiba
au kuwapa yale ambayo serikali inawachagulia wananchi ili wasome.
Padre wa Kanisa Katoliki aliyekuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha
Mtakatifu Augustino Dk. Joseph Matumaini amesema, “Idara ya Habari
Maelezo imepitwa na wakati, hivyo ifutwe au kama haitafutwa vyombo vya
habari viunde chombo kiingine kitakachotenda haki ili kuiacha idara hii
kwa maslahi ya serikali ambayo yameonekana kuwa sio maslahi ya umma.”
CHANZO TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment