HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni imejikuta njia panda baada
ya kutakiwa kulipa sh 695,520,000 kwa waliokuwa wakazi wa Magomeni
Kota ikiwa ni pango la kodi kuanzia Januari hadi Desemba mwaka huu.
Halmashauri hiyo iliingia mkataba na wakazi hao Septemba mwaka 2011
katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi ambapo ilikubali kuwalipia pango
la chumba wakazi hao kuanzia mwaka huu hadi pale nyumba za eneo hilo
zitakapokamilika.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano, mmoja wa watendaji wa
halmashauri hiyo ambaye hakupenda jina lake litajwe, alisema kuwa
malipo hayo yamesababisha migongano baina ya viongozi wa manispaa na
baraza la madiwani.
Alisema kuwa kuliibuka mvutano mkubwa katika kikao cha baraza la
wadiwani ambapo baadhi walipinga mkataba huo na wameshauri malipo hayo
yasitishwe ili hatua za kisheria zichukuliwe.
“Hivi ninavyokwambia kuna sintofahamu juu ya malipo hayo maana wakazi
hao wana mkataba halali unaotambuliwa na mahakama na hata baraza la
madiwani linafahamu hilo ndiyo linajaribu kupigania mkataba huo uvunjwe
ili fedha hizo zitumike kwa shughuli nyingine,” alisema.
Alisema kuwa mbali na baraza la madiwani wapo watendaji wa juu wa
halmashauri hiyo ambao nao hawakubaliani na mkataba huo na kutaka
uvunjwe kwa kuwa sio busara kwa manispaa hiyo kuwalipia pango wakazi
wake.
Hata hivyo akizungumza na gazeti hili jana kiongozi wa kamati ya
wakazi hao, Abbas Mkweta, alisema kuwa halmashauri inapaswa kutambua na
kuuthamini mkataba waliosaini na wakazi hao juu ya kuwalipia malipo
hayo.
Mkweta alisema kuwa halmashauri ilipaswa kuwa imelipa malipo hayo
tangu Januari mwaka huu lakini ikatoa udhuru na kuomba kulipa fedha
hizo ifikapo Septemba mwaka huu.
“Hapa tulipo tunaendelea na uhakiki wa majina ya waliokuwa wakazi wa
eneo hilo na zoezi hilo lilianza juzi na linakamilika leo,” alisema.
Alisema kuwa mkataba huo ni halali na ni makubaliano yaliyofanyika
kisheria hivyo hakuna haja ya watendaji wa halmashauri hiyo kusigana
juu ya malipo hayo.
Mkweta aliongeza kuwa manispaa hiyo ilijizatiti kulipa malipo hayo
iwapo itashindwa kukamilisha ujenzi wa nyumba katika eneo hilo ili
kuwawezesha kuingia katika nyumba hizo.
“Sasa kama nyumba walizosema wanajenga hazijakamilika na mkataba
unaitaka halmashauri itulipie kodi wanachopinga nini wakati hayo ni
makubaliano…tulikubaliana sisi tupewe kipaumbele katika nyumba hizo
kama zingekamilika na tungekuwa tunalipa kodi ya sh elfu 90,000 kwa
mwezi na kwa mwaka tulipaswa kulipa sh milioni 1,080,000,” alisema.
Alisema kuwa wakazi hao hawana haja na fedha hizo wanachohitaji ni
halmashauri hiyo kutekeleza makubaliano ya kujenga nyumba hizo ili
waweze kupanga na kuondokana na usumbufu.
Nyumba za magomeni kota zilijengwa na jiji la Dar miaka ya 1950 na baadaye kumilikishwa kwa halmashauri ya manispaa hiyo.
Nyumba hizo zilipangishwa kwa mkataba kwa wakazi hadi mwaka 2006.
Wakazi hao 644 waliendelea kukaa hapo hadi 2009 ambapo walitakiwa
kuondolewa na wakakimbilia mahakamani.
CHANZO TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment