CHANZO: GLOBAL PUBLISHERS
Aliyekuwa Shehe Mkuu wa Bakwata Wilaya ya Mbeya, Abubakar Mketo amefariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita kufuatia kuanguka ghafla makaburini wakati akitoa mawaidha ya Kiislam ya jinsi waumini wanavyotakiwa kuishi katika ulimwengu wa dhambi! Inauma sana!
Tukio hilo lililowaacha watu na machozi lilijiri katika Makaburi ya Nonde jijini hapa wakati wa mazishi ya marehemu aliyejulikana kwa jina la Mayasa Salmini au Bibi Majuto aliyefariki dunia katikati ya wiki iliyopita.
ILIVYOKUWA
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, baada ya kumaliza kuusitiri mwili wa marehemu Bibi Majuto ndani ya nyumba yake ya milele, Shehe Mketo alisimama na kuanza kutoa mawaidha kwa waombolezaji waliohudhuria mazishi hayo akiwaelekeza namna ya kuishi kwa kutii amri za Mungu na kufuata njia zake kwa vile hakuna anayejua atakufa lini kama ilivyokuwa kwa marehemu Bibi Majuto.
HEBU MSIKIE
Vyanzo vinadai kuwa, dakika chache kabla ya shehe huyo hajapatwa na mauti alionekana ni mwenye afya njema huku akitoa Neno la Mungu ambalo kila mtu aliyekuwa eneo hilo la makaburi lilimgusa na kujitafakari upya njia zake, alisema:
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abasi Kandolo akiwa kwenye mazishi.
“Kila nafsi lazima itaonja mauti na si ajabu hata mimi ninayeongea
wakati huu naweza kufa wakati wowote ule baada ya kumaliza mazungumzo
haya mbele ya macho yenu sasa hivi.”KUANGUKA
Mashuhuda wanasema kweli kifo kiko mwilini mwa mtu kwani mara baada ya kumaliza kusema maneno hayo, Shehe Mketo aliyesifika kwa uadilifu alianguka chini ghafla na hapo hekaheka zikaanza, watu wakiulizana ‘jamani nini kimetokea, jamani nini kimetokea?’
AKIMBIZWA HOSPITALI KUMBE TAYARI
Baadhi ya watu walimbeba shehe huyo huku wakimpepea na kumwingiza kwenye gari kisha kumkumbiza Hospitali ya Rufaa ya Mbeya ambako madaktari baada ya kumpokea walisema shehe huyo tayari alikuwa ni marehemu.
MSIBA WAKE
Shehe aliyekuwa akitoa mawaidha wakati wa mazishi sasa ukawekwa msiba wake, watu wakaanza kuomboleza nyumbani kwake Soko Matola jijini hapa ambako pia msiba wa Bibi Majuto ulikuwepo huku kila mmoja akiuliza nini kilimpata mtumishi huyo wa Mungu mpaka akapoteza maisha baada ya kauli yenye mwashirio wa tukio hilo?
MAZISHI YAKE PALEPALE
Kesho yake, mchana shehe huyo ambaye saa ishirini na nne nyuma alikuwa hai, alizikwa kwenye makaburi yaleyale aliyotolea mawaidha ya Bibi Majuto ambapo kaburi lake limepakana na la bibi huyo.
KAULI ZA MASHEHE
Mashehe mbalimbali waliohudhuria mazishi hayo walisema kifo cha mwenzao kinafundisha waumini kujiandaa na safari ya kifo ambacho kinaweza kutokea wakati wowote bila kutarajia.
Shehe wa Msikiti wa Isanga, Ibrahim Bombo yeye alisema: “Tukio hili ni dalili pekee ambazo zinapaswa kuwafundisha waumini wa Kiislam kujiandaa kwa kufanya matendo mema kwa kuwa kifo kinaweza kumkuta binadamu mahala popote.
“Tujiwekee maandalizi ya safari ya akhera, hakuna anayejua saa wala tarehe ya kuondoka kwake duniani, kifo cha shehe wetu kitupe mafundisho.”CHA AJABU SASA
Cha ajabu sasa, wakati shehe huyo anasema hayo, baadhi ya waombolezaji walimtolea macho pima, huenda waliamini kitampata kilichompata marehemu!
KAULI YA MKUU WA MKOA
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro aliwataka ndugu, jamaa, marafiki na waumini kutohusisha kifo hicho na imani zozote za kishirikina bali waamini kuwa kimetokana na mipango ya Mungu kwa vile kila mtu ataondoka duniani kwa njia zake.
No comments:
Post a Comment