Kutokana na hatua ya Samson Mwigamba, aliyesimamishwa uenyekiti wa
CHADEMA Mkoa wa Arusha, kukiri mbele ya waandishi wa habari kuwa amevunja
katiba, kanuni, maadili, miongozo, taratibu na itifaki za chama kwamba yeye
ndiye aliyeandika (kwa kutumia jina bandia);
Kwenye mitandao ya kijamii, waraka uliojaa uongo, upotoshaji na
uchonganishi kwa wanachama na viongozi, Idara ya Habari ya CHADEMA (kupitia
Ofisa Habari, ambaye alikuwepo kwenye kikao hicho) imechukua hatua ya kuanza kutoa
na kuandaa utolewaji wa taarifa rasmi zinazojibu uongo, upotoshaji na
uchonganishi ulioandikwa na Mwigamba, ili kuweka kumbumbu sawa, wanachama na
Watanzania wote waelewe.
Kwa kuanzia, leo tunatoa ufafanuzi juu ya suala la kikatiba la
ukomo wa uongozi ndani ya chama.
Kupitia taarifa hii ya Idara ya Habari, kwanza tunapenda
kushangazwa na hatua ya Mwigamba kuendelea kuvunja katiba, kanuni, maadili,
miongozo, taratibu na itifaki ya chama, ambapo kupitia vyombo vya habari
ameendelea kutunga mambo yasiyokuwepo badala ya kuwasilisha hoja zake (kama
anazo) kupitia vikao halali vya chama ambavyo yeye anao uwezo wa kuitisha au
kuhudhuria.
Tungependa umma ufahamu masuala kadhaa, kwamba katika kikao cha
Baraza la Uongozi wa Kanda ya Kaskazini (Tanga, Manyara, Kilimnajaro a Arusha),
muda mfupi kabla Mwigamba hajatuhumiwa kwa usaliti na hujuma, alikuwa ametoka
kuwasilisha taarifa ya hali ya chama katika mkoa wa Arusha.