Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amethibitisha kutokea kwa kifo hicho, hata hivyo hakuwa tayari kuelezea kwa undani kwa madai kuwa taarifa hizo zimemfikia sasa hivi.
Mmoja wa watoto wa Komba ambaye aliyejitambulisha kwa jina la Herman amethibitisha kutokea kwa msiba huo na akasema, huku akilia, msiba wa baba yake upo nyumbani kwake Mbezi Tangi Bovu, Dar.
Habari zinasema asubuhi ya leo Komba alikwenda kwenye shughuli zake za kikazi kama kawaida lakini baadaye akajisikia vibaya, hivyo akaamua kurudi nyumbani ambako alizidiwa ndipo familia yake ilipoamua kumkimbiza Hospitali ya TMJ lakini alipopimwa na madaktari ikathibitika kuwa alikuwa tayari ameaga dunia. habari zaidi zinasema kuwa hivi sasa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Jeshi ya Lugalo.
Kapteni Komba ambaye pia ni Mkurugugenzi wa Kikundi cha Maigizo cha Tanzania One Theatre (TOT), ambacho kina kikundi cha taarabu na bendi inayokwenda na mtindo wa Achimenengule, amekuwa akikisaidia sana chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kampeni zake wakati wa uchaguzi kwa kutunga nyimbo za kuhamasisha wapiga kura na kushiriki kupiga live kwenye majukwaa ya kisiasa.