NITAELEWEKA tu! Sina ubishi kwamba kwa sasa Bongo, fani ya sanaa ya
uigizaji ndiyo imeshika kasi kukubalika katika jamii (anayebisha
anyooshe mkono, najua hakuna).
Elizabeth Michael 'Lulu'.
Siku hizi ukikatisha kwenye mitaa mbalimbali nchini Tanzania, hasa
uswahilini, utagundua wengi wanaangalia ‘filamu za akina Kanumba’ kama
vile Uncle JJ, Ndoa Yangu, Mr. Ben, World of Benefit na nyingine nyingi.
Haya ni maendeleo kwa wasanii wetu ambao zamani walikuwa wakihaha
kutoka lakini walishindwa kutokana na soko la filamu Bongo kushikwa na
‘muvi za akina Rambo’ na baadaye akina Noa Ramsey.
ANGALIZO LANGU
Pamoja na yote hayo, kuna
angalizo langu. Ili sanaa hiyo izidi kukua nchini ni lazima kuwe na
ushirikiano mkubwa kati ya wasanii wenyewe (waigizaji) na vyombo vya
habari.
Aunt Ezekiel.
Vyombo vya habari ndivyo vinavyotangaza kazi zao mpaka zikajulikana
na akina mama Nyakomba kule kijijini Songea (nyumbi hii, bomba hii).
Lakini kumekuwa na ugumu wa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya
waigizaji, hasa wale ambao wanajiita (hawaitwi) wanajiita masupastaa au
mastaa wa Bongo (Bongo Movies).
Hawa jamaa baada ya kuamini wamekuwa na majina makubwa kupitia filamu
(ni vyombo vya habari vilivyowafanya wawe na majina makubwa) wamekuwa
na dharau, wamekuwa bize, wamekuwa hawana nafasi, simu wamekuwa
wakiziweka mbali na wao walipo au hazina chaji tangu jana usiku (si
unajua umeme wa Tanesco?).
Jack Wolper.
MBAYA ZAIDI
Mbaya zaidi, hao ‘mastaa’ wapo hata
wale waliokwishaonekana kwenye filamu tatu tu tena si ‘mastering’,
waliigiza kwenye udereva, kufungua mageti, wakaribisha wageni maofisini
au wasaidizi wa kazi za ndani ‘mahausigeli’.
NINAVYOJUA MIMI
Kwa mujibu wa ufahamu wangu
mdogo ni kwamba, katika kila tasnia duniani kuna masupastaa na mastaa.
Pia wapo wahusika wa fani husika. Kama filamu tunasema waigizaji.
Sasa hawa wa Bongo ambao nao pia wamejiweka kwenye kundi la masupastaa
na mastaa wananitatiza kila kukicha, kwamba ni wagumu kupatikana, iwe
laivu au kwa simu kwa sababu wao ni maarufu katika fani.
Jacob Steven 'JB'.
MASUPASTAA
Kufuatia lawama zangu hizi kwa
wasanii wa fillamu Bongo, kama mtu ataniuliza ninavyojua mimi nani
supastaa, staa na mwigizaji orodha yao ninayo na niko tayari kuiweka
wazi.
Siwezi kusema Ray, JB, Aunt Ezekiel, Nora, Wolper, Johari,
Natasha, Monalisa, Dk. Cheni, Riyama Ali, Lulu, Mzee Majuto, Mzee Small
siyo mastaa wa filamu Bongo.
Wamecheza filamu nyingi, wamejenga majina makubwa kupitia sanaa hiyo.
Japokuwa miongoni mwao wapo ambao ni wababaishaji kwenye kupokea simu
na kujifanya ‘aghali’ kupatikana.
Lakini pia kuna kundi la mastaa wa
filamu za Bongo; hawa ni akina Baba Haji, Kuambiana, Maya, Jini Kabula,
Wastara, Mr. Chuz, Frank Mwikonge, Mzee Chilo, Mzee Magali, Cloud,
Penina, Richie, Bi. Chau na Thea.
Wengine ambao kwangu ni mastaa ni, Jack wa Chuz, Cathy, Lucy Komba,
Big, Chekibudi, Baba Haji, Kelvin, Odama, Rose Ndauka, William Mtitu,
Tino, Flora Mvungi, Nisha, Shilole, Mainda, Shamsa Ford, Snura, Mlela,
Shumileta, Hemed, Yusuf Mlela, Dude na Maya.
Mbali na makundi hayo, kuna ambao wamepitiliza usupastaa na sasa
wameingia kwenye kundi la wakongwe wa sanaa. Hawa ni kama akina Natasha,
Mzee Small, Mzee Majuto, Bi. Hindu, Bi. Mwenda, Bi. Chau, Kemmy na
Muhogo Mchungu.
Mzee Majuto.
Lakini napata tabu kusema, Batuli, Zamda, Tiko, Slim, Skaina, Rachel
Haule, Chikoka, Kupa, Mafufu, Badra na wengine wengi ambao kwenye fani
hawana hata mwaka mmoja ni mastaa.
Kwa nchi za wenzetu ‘majuu’,
vyombo vya habari havitambulishi kila mwigizaji kama staa, ila wanakuwa
mastaa katika filamu walizocheza tu, hususan kama amecheza filamu mbili
au tatu.
Mfano; wakitaka kumtambulisha Rachel Haule watasema: “Staa wa filamu
ya…..(wataitaja jina), Rachel Haule amepata mchumba (mfano lakini).
Majuu staa, kama wa filamu ni yule aliyekwishacheza muvi zaidi ya 10
akiwa ni stering na zikatikisa. Kibongobongo, hata akicheza filamu moja
halafu akavuma sana, tena wengine huvuma kwa mambo nje ya filamu, ni
staa.
Makala haya ni mtazamo wangu.