Awali ya yote naanza kwa kutoa mkono wa pole kwa wapenda burudani kote
nchini kutokana na misiba ya wasanii iliyofuatana, jambo lililoipelekea
kuwa na majonzi yasiyokoma.
Awali alianza Maria Khamis ‘Paka Mapepe’ aliyekuwa muimbaji wa muziki
wa taarab wa kundi la Tanzania One Theatre (TOT) aliyefariki kutokana
kifafa cha uzazi.
Wakati watu wakiwa hawajakaa sawa wala machozi kufutika vema usoni au
kwa msemo mwingine naweza kusema ikiwa bado tanga halijaanuliwa sawasawa
tasnia ya filamu ikaondokewa na Khalid Mohamed a.k.a Mlopelo (41)
aliyeng’ara na kikundi cha Kaole kilichokuwa kikirushwa na kituo cha
televisheni cha ITV ambako ndiko alikopata umaarufu wake na hatimaye
kushirikishwa katika filamu kadhaa.
Wakati msiba wa Mlopelo haujaisha msanii mwingine wa Bongo Movie
John Maganga akafariki Jumamosi iliyopita na kuzikwa Jumanne wiki hii.
Wakati kukiwa kuna msiba wa Maganga Jumatatu usiku msanii Ramadhan
Mkiteti alipata ajali maeneo ya Maguzoni Muheza mkoani Tanga.
Hakika wasanii na tasnia wamekumbwa na misiba yote ya uchungu; nachukua fursa hii kuwapa pole.
Ni kweli hakuna msiba unaozoeleka hata siku moja kama babu au bibi yako amefariki miaka kadhaa iliyopita, inauma sana.