Muungano wa Afrika umeituhumu mahakama ya kimataifa ya ICC kwa kuwaandama wafrika kwa sababu ya rangi yao.
Waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn aliyasema hayo akiongeza kuwa italalamika mbele ya Umoja wa Mataifa kuhusu hilo.
Rais Kenyatta anatarajiwa kufika mbele ya
mahakama hiyo mwezi Julai kusikiliza mashtaka dhidi yake kuhusu uhalifu
dhidi ya binadamu.
Aidha Kenyatta amekanusha tuhuma hiuzo ambazo
zinatokana na madai ya kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi Kenya mwaka
2007 ambapo maelfu walipoteza maisha yao na wengine kuachwa bila makao.
Alichaguliwa kama Rais katika uchaguzi
uliofanyika mwezi Machi na kumshinda mpinzani wake mkubwa Raila Odinga
katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali.
Akihutubia kikao cha marais wa Afrika kwenye
mkutano wa AU mjini Addis Ababa , bwana Hailemariam alisema kuwa
viongozi wa Afrika wameelezea wasiwasi kuwa asilimia 99 ya wale
wanaotakikana na mahakama ya ICC kwa makosa yoyote yale ni waafrika.
"hii ni dalili ya kuwa mambo sio sawa, mfumo wa ICC una hujuma,'' alisema bwana Hailemariam
Mahakama ya ICC ilibuniwa ili kuangamiza kile
kilichoonekana kuwa viongozi wanaofanya uhalifu bila kujali, lakini
sasa ''mfumo huo umegeuka na kuwa mfumo wa kuwaandamana watu kwa misingi
ya rangi,'' alisema bwana Hailemariam.