WAKATI baadhi ya wanasiasa wakiwa wameanza kujiwinda kwa ajili
ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, Shirika la Utafiti la
Synovate limetoa matokeo ya utafiti wake ambao unaonyesha vigogo tisa
kuwamo katika mchuano huo.
Utafiti huo umeonyesha kuwa endapo uchaguzi
huo ungefanyika sasa, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Dk Willibrod Slaa angeibuka mshindi baada ya kuongoza orodha
hiyo akipata asilimia 17.
Katika matokeo ya utafiti huo uliofanywa
Desemba mwaka jana, Dk Slaa anafuatiwa kwa mbali na Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda ambaye amefungana na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe
kila mmoja akipata asilimia tisa.
Hata hivyo, licha ya kuongoza, Dk Slaa
ameporomoka kwa asilimia 25 ikilinganishwa na matokeo ya utafiti kama
huo uliofanywa na taasisi hiyo mwaka 2011 ambapo alipata asilimia 42.
Kadhalika, umaarufu wa Pinda ambaye anaongoza
miongoni mwa wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), umeshuka kwa
asilimia tatu kutoka 12 za mwaka juzi, wakati Zitto ameendelea na
kiwango kilekile cha asilimia tisa alizopata katika utafiti
uliotangulia.
Wengine wanaofuata na asilimia walizopata kwenye mabano
ni Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli (8), Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa (7) na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba (5).
Pia wamo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe (4) ambaye amefungana na Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe (4) na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Samuel Sitta (2).
Ikilinganishwa na utafiti wa 2011, Lipumba ameporomoka kwa asilimia tisa.
Lowassa
amepanda kwa asilimia sita, Dk Magufuli asilimia nne, Mbowe na Membe
wamepanda kwa asilimia mbili kila mmoja, wakati Sitta amebaki katika
kiwango kilekile cha asilimia mbili.