WASHIRIKI 20 wa shindano la kuimba la Epiq Bongo Star Search
(EBSS), wanatarajia kuingia kambini hivi karibuni jijini Dar es Salaam
ili kuanza mafunzo rasmi yatakayofanikisha kupata washiriki bora katika
shindano hilo linalotarajiwa kufikia fainali Novemba 17, mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Benchmark Productions
Limited, ambao ndio waandaaji wa EBSS, Madam Ritha Poulsen, alisema
shindano la mwaka huu linatarajiwa kuwa la aina yake kutokana na jinsi
walivyojipanga na kupata washiriki wenye uwezo kutoka mikoani na jijini.
Ritha alisema wameazimia kuingia kambini mapema ili kuwapa fursa
washiriki kujifunza zaidi na kuwa na uwezo wa kutosha, ambao utazalisha
waimbaji wazuri katika tasnia ya muziki hapa nchini, kupitia kituo cha
runinga cha TBC1.
“Mwaka huu washiriki ni wengi, ila tumewapata 20 bora na kutokana na
mambo ya kibiashara, kwa sasa EBSS itakuwa inarushwa TBC1 kila Jumapili
saa tatu usiku na marudio Jumatano saa 8 mchana, badala ya ITV, kuhama
kwetu hakuna ugomvi wala nini ni mambo ya kibiashara, kwani nimeanza
kusikia maneno mengine hususan kwenye ‘social media’, sisi hatuko huko,
tuko kibiashara zaidi, zaidi ya hapo hakuna,” alisema Ritha.
Naye Balozi wa EBSS, mshindi wa mwaka jana, Walter Chilambo,
aliwashukuru vijana kujitokeza kwa wingi katika mikoa mbalimbali ambayo
wametembelea, hususan vijana wa kike, ambao walikuwa hawajitokezi kwa
wingi.