LOS ANGELES, MAREKANI
HAKUNA shabiki wa muziki ambaye anaweza kutoka mbele na kusema halifahamu jina la Rihanna.
Nyota huyo mwenye sauti tamu na sura ya kupendeza, anawika duniani kote na amekuwa akivuna mashabiki kila kukicha.
Mashabiki wanavyoongezeka ndivyo dada huyo
aliyezaliwa miaka 25 iliyopita huko Saint Michael, Barbados anavyoongeza
utajiri, hiyo ni kwa kuwa nakala za albamu zake hununuliwa zaidi.
Kwa mujibu wa mtandano wa The Richest, Rihanna
ambaye pia ni mwigizaji, ana utajiri wa dola 60 milioni mpaka kufikia
Desemba 2012.
Awali mwanamuziki huyo alikuwa hafahamiki, lakini
maisha yake yalibadilika baada ya rafiki yake mmoja kumkutanisha na Evan
Rodgers, prodyuza kutoka New York.
Prodyuza huyo alikuwa katika mapumziko ya kawaida huko Barbados akiwa na mke wake ambaye ni mwenyeji wa eneo hilo.
Baada ya kutambulishwa, Rodgers alimsikiliza na
alikubali kuwa mwanamuziki huyo ni mkali na alimtaka afike New York ili
akutane na Jay-Z, ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya kurekodia ya Def
Jam.
Jay-Z alimsikiliza anavyoimba na kufahamu kuwa
Rihanna hakuwa na sauti ya kawaida, alikuwa na nyota ya pekee. Wakati
huo alikuwa na miaka 16 tu lakini alisaini mkataba na Kampuni ya Def
Jam.