CHAMA Cha Mapinduzi kimekitabiria kifo Chadema baada ya uchaguzi
waa 2015 kikieleza kuwa CCM ikishinda, chama hicho kitakuwa hakina
nguvu tena kwa kuwa Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa atakuwa
amechoka.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba
aliliambia gazeti hili jana kuwa chama hicho kinapoteza umaarufu kadri
siku zinavyokwenda hasa kutokana na siasa zake za uchochezi na mwaka
2015 ndio itakuwa mwisho wa chama hicho.
Alisema kitakufa na kitasahaulika kabisa,
akisema sasa hivi vijana wameshaanza kuwakimbia, na kwamba anaamini pia
baada ya 2015 hakuna diwani ambaye atagombea kupitia chama hicho.

Alisema pia ni mwaka ambao Katibu wa Chadema
Willibrod Slaa amestaafu kwa kuwa alishatangaza asiposhinda atastaafu na
Chadema haiwezi kushinda hivyo mwisho wa Dk Slaa ndio utakuwa umefika
kwa kuwa nyota yake haitang’aa tena.
“Nguvu ya Dk Slaa aliyokuwa nayo miaka miwili
iliyopita sio aliyonayo sasa na mpaka mwaka 2015 atakuwa ameisha
kabisa.”alisisitiza.
Pia Mwigulu aliyataka makundi yaliyojichomoza
ndani ya CCM ikiwa ni harakati za kuwania urais mwaka 2015 kuheshimu
ilani ya chama hicho kwa kuitekeleza na kuisimamia kwa kutoleta vurugu
ndani ya chama wala kujenga chuki kwa wale ambao hawawaungi mkono.