Tofauti na ilivyo katika fani nyingine, wasanii wamekuwa wakijibatiza majina ya ziada (a.k.a). Mbaya zaidi, majina hayo huwa yanaanza kama utani lakini inafika wakati msanii husika analizoea jina hilo jipya na kulifanya kuwa kama rasmi.
LULU
Jina lake halisi ni Elizabeth Michael, Lulu lilizoeleka kupitia tasnia ya uigizaji. Alianza kulitumia wakati alipojiunga na Kundi la Sanaa la Kaole.
Hadi leo hii, siyo rahisi kabisa mtu kutokea na kumuita jina la Elizabeth, wengi wanamfahamu kwa jina la Lulu.
RAY
Ray ndiyo jina ambalo limezoeleka na wengi. Vincent Kigosi alilopewa na wazazi wake ni kama limekufa. Kwa zaidi ya miaka kumi sasa tangu alipokuwa kwenye Kundi la Sanaa la Kaole hadi sasa.
Jina la Ray ndiyo watu wanalolifahamu zaidi ingawa hivi karibuni baadhi ya wasanii wenzake wamekuwa wakijaribu kumuita Vincent ili kurudisha uhai wa jina hilo.
JOHARI
Jina lake halisi ni Blandina Chagula. Johari lilizaliwa kwenye Tamthiliya iliyobeba taito ya jina hilo. Akiwa katika Kundi la Kaole, alianza kujiita Blandy, baadaye alibadilisha jina hilo na kuwa Johari walipoingiza tamthiliya hiyo ambayo pia ilizaa filamu.
“Kuna wakati huwa najuta kutumia jina la a.k.a ambalo limefunika kabisa jina langu la asili,” anasema Johari.
DK. CHENI
Ameanza gemu kitambo, tangu Kundi la Splended. Jina alilopewa na wazazi wake ni Mahsein Awadhi, kwa sasa limekufa. Hakuna anayelitumia, hata yeye mwenyewe.
Jina hilo lilizaliwa baada ya mazoea yake ya kupenda kuvaa cheni kubwa kwenye michezo iliyokuwa ikirushwa Runingani, kwa sasa wengi wanashindwa hata kulitamka jina lake.