BINAFSI nafahamu kwamba Irene Uwoya aliwahi kuwa staa mkubwa nchini
lakini akafanya makosa na sasa ameshuka chati. Ameporomoka kwa kiasi
kikubwa sana.
Irene Uwoya.
Elizabeth Michael ‘Lulu’, baada ya ‘ajali’ yake na marehemu Steven
Kanumba, alikaa mahabusu kwa zaidi ya mwaka mmoja lakini baada ya kutoka
ameonekana kuwa na mafanikio makubwa kuliko Uwoya ambaye siku zote yupo
mtaani.
Pengine kuna aina fulani ya maisha ambayo Uwoya
amejichagulia maana akina Rose Ndauka, Aunt Ezekiel, Wema Sepetu na
wengineo wamekuwa wakifanya vizuri, wanamfunika sana. Ameshindwa
kujisahihisha, ataendelea kusugua.
Najua kwamba Uwoya ana hali mbaya
kisanii, amechoka, muonekano wake hausisimui tena, amepoteza mashabiki,
kwa maana hiyo hauzi. Dili za kucheza filamu zinaota mbawa kila kukicha,
maprodyuza wanataka wakali ambao wanafanya biashara sokoni.
Naelewa
kuwa hivi sasa katika ulimwengu wa masupastaa, Uwoya amebaki
msindikizaji lakini sikuwahi kufikiri kwamba anaweza kufikia hatua mbaya
kiasi hicho. Kafikishwa mbaroni kwa wizi wa simu? Yaani wizi wa simu ya
mkononi! Anatia huruma.
Yamemfika yapi? Sitaki kuamini kama Uwoya
anashindwa kununua simu halali. Akili nyingine inaniambia kuwa hawa dada
zetu wanaharibiwa na uchu wa kupenda vitu vya juu lakini uwezo ni
mdogo. Je, huo wizi wenyewe alifanyaje?
Atakapofikishwa mahakamani
pengine itajulikana kama kweli amehusika na wizi huo, basi itafahamika
ameufanyaje. Ni yeye moja kwa moja au kupitia kwa mtu mwingine? Dunia
ina mengi, ni vizuri hili jambo likafika kortini, huko tutajua ukweli
halisi.
Swali langu ni hili, kama kweli ile simu alinunua kwa nini
pale kituoni hakutoa risiti? Hata kama ingekuwa nyumbani, alishindwa
nini kuagiza aletewe kuthibitisha kama ni mali yake? Maswali hayo mawili
yanaongeza uzani kwenye madai kwamba ile simu ni ya wizi.
Ni ya wizi
sawa, je, ni kweli Uwoya anaweza kuiba simu? Inawezekana kabisa akatega
Kariakoo halafu amvizie mtu na kumchomolea? Maana mashtaka dhidi yake
ni Wizi wa Maungoni, yaani wizi wa kumchomolea mtu kitu kutoka mwilini.
Kesi
ipo Msimbazi Polisi na imeandikwa kwenye kitabu cha ripoti za
kumbukumbu (report book ‘RB’) kwa nambari MS/RB/8522/2013. Hata hivyo,
simu yenyewe iliyoibwa ina thamani kubwa, nahisi Uwoya aliinunua kwa mtu
ambaye ndiye mwizi.
Mikono ya Uwoya na vidole vyake vilivyo,
haoneshi kama anaweza kuwa mkali wa kuchomolea watu. Hata kama kaishiwa
na kupigika, siyo rahisi akafanya hivyo. Sura yake haioneshi ushujaa wa
‘kupiga ndole’ lakini ya Mungu mengi.