HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWA WANANCHI, TAREHE 4 OKTOBA, 2013
Ndugu Wananchi;
Namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kumaliza mwezi Septemba salama na kuwasiliana kwa kutumia utaratibu wetu huu mzuri. Naomba radhi kuzungumza nanyi siku ya leo kwa sababu nilikuwa safari na nilirejea jioni ya tarehe 30 Septemba, 2013. Awali nilifikiria nisiseme, nisubiri mwisho wa mwezi wa Oktoba. Lakini, baada ya kupata taarifa ya yaliyojiri, nimeshauriwa na nimekubali angalau niyasemee baadhi ya mambo huenda itasaidia. Niwieni radhi nisipoyasemea baadhi ya mambo siyo kwa kuyapuuza, bali kwa kuepuka hotuba kuwa ndefu mno. Nitayatafutia mahali pengine pa kuyasemea.
Uhusiano na Rwanda
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi wa Julai, nilizungumzia hali ya uhusiano wetu na Rwanda kutokuwa mzuri na tatizo la ujambazi na wahamiaji haramu katika Mikoa ya Kigoma, Geita na Kagera. Nafurahi kusema kuwa kwa yote mawili kuna maendeleo ya kutia moyo.
Tarehe 5 Septemba, 2013, nilikutana na kuzungumza na Mheshimiwa Rais Paul Kagame wa Rwanda mjini Kampala. Tuliitumia fursa ya ushiriki wetu katika Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu kuzungumzia uhusiano baina yetu na nchi zetu. Mazungumzo yalikuwa mazuri na sote tulikubaliana kuwa yaliyopita si ndwele tugange yajayo. Kwa sababu hiyo tulielewana kuwa tutengeneze mazingira yatakayosaidia kutuliza hali na kurudisha nchi zetu katika uhusiano mwema kama ilivyokuwa siku zote. Nawaomba ndugu zangu hususan wanasiasa, watumishi wa umma, wanahabari na wenye mitandao ya kijamii na blog na wananchi kwa ujumla tusaidie kuimarisha uhusiano mwema baina ya Rwanda na Tanzania na watu wake.
Majambazi na Wahamiaji Haramu
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba hiyo pia nilisema kuwa tutachukua hatua thabiti dhidi ya majambazi na wageni wanaoishi nchini bila ya kuzingatia taratibu zinazohusika. Niliwataka majambazi wajisalimishe wao na silaha zao kwa hiari. Wale wanaoishi nchini bila ya kuwa na kibali halali wahalalishe ukaazi wao au warejee makwao. Nilitoa siku 14 kuanzia tarehe 29 Agosti, 2013 wafanye hivyo kwani baada ya hapo tungeanzisha operesheni maalum ya kushughulika na watu wa makundi yote mawili.
Ndugu Wananchi;
Kumekuwepo na mafanikio ya kutia moyo. Kwa upande wa wahamiaji wanaoishi nchini kinyume cha sheria watu wapatao 21,254 waliondoka kwa hiari. Hali kadhalika zaidi ya ng'ombe 8,000 waliondolewa na silaha 102 zilisalimishwa. Baada ya operesheni kuanza tarehe 6 Septemba, 2013 na kumalizika tarehe 20 Septemba, 2013, wahamiaji haramu 12,828 walirejeshwa makwao na watuhumiwa 279 wa unyang'anyi wa kutumia silaha walikamatwa. Aidha, mabomu 10 ya kutupa kwa mkono (offensive hand grenades), silaha 80, risasi 780 na mitambo 2 ya kutengeneza magobole vilikamatwa. Pia, ng'ombe 8,226 walikamatwa wakichungwa katika mapori ya hifadhi. Kwa upande wa mazao ya misitu, mbao 2,105 zilikamatwa pamoja na nyara mbalimbali za Serikali.
Ndugu Wananchi;
Agizo la kuwataka watu wanaoishi nchini isivyo halali wahalalishe ukaazi wao au waondoke kwa hiari au wataondolewa lilipotoshwa hasa na vyombo vya habari vya nje ya Tanzania. Walikuwa wanadai eti Tanzania ilikuwa inafukuza wakimbizi. Madai hayo si ya kweli hata kidogo. Hadi kufikia tarehe 30 Septemba, 2013 wakimbizi 68,711 walikuwepo kwenye Kambi ya Nyarugusu, Mkoani Kigoma. Hakuna mkimbizi ye yote aliyetakiwa kuondoka. Ukweli ni kwamba hakuna mtu ye yote kati ya wale watu walioondoka kwa hiari au kusaidiwa kuondoka wakati wa operesheni ambaye ni mkimbizi. Kama ingekuwa hivyo, wa kwanza kulalamika wangekuwa wenzetu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa. Bahati nzuri jambo hilo halikutokea.