HATIMAYE ujenzi wa kiwanda cha kusafisha gesi kabla ya kusafirishwa kwenda Dar es Salaam umeanza mkoani Mtwara.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,
Eliakim Maswi alisema jana kuwa ujenzi huo unaofanywa na Kampuni ya
China Petroleum and Technology Development Co-operation (CPTDC), ambao
awali, ulipaswa kuanza wiki iliyopita, umeanza juzi baada ya Serikali
kufikia mwafaka na wananchi wa Kijiji cha Msimbati kinapojengwa.
“Mkuu wa Wilaya ya Mtwara (Wilman Ndile) na vijana
wake walilazimika kufika Kijiji cha Msimbati, ambako wananchi walikuwa
na mgogoro na watu wa Marine Park,” alisema Maswi.
Alisema baada ya ziara hiyo kushindwa kufanyika
Jumapili iliyopita, uongozi wa wilaya ulikutana na viongozi wa kijiji na
kufikia mwafaka uliofanikisha kuanza kwa ujenzi huo.
Alisema kuanzia mradi huo kutatoa ajira za kawaida
kwa wakazi saba wa maeneo yanayozunguka mradi huo na kwamba kazi hiyo
itaongeza mahitaji ya bidhaa mbalimbali na huduma katika Kata ya
Msimbati
“Mathalan kuku, matunda na mboga za majani
vinahitajika sana. Sasa wananchi ambao awali, hawakutaka kuelezwa
lolote, wameanza kuchangamkia fursa hizo jambo ambalo litawanufaisha
zaidi,” alisema.