HATIMA ya mawaziri watano kuendelea na nyadhifa zao iko shakani
baada ya wabunge kuwatuhumu kushindwa kuwajibika ipasavyo na
kusababisha migogoro ya wafugaji na wakulima.
Kufuatia kadhia hiyo iliyojitokeza wakati wa kutekelezwa kwa
Operesheni Kimbunga na Operesheni Tokomeza Ujangili, Bunge limeamua
kuunda kamati teule kuchunguza migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo
imesababisha vifo, ukiukaji wa haki za binadamu na upotevu wa mali.
Wabunge wengi waliochangia hoja hiyo waliwataja wazi mawazi kadhaa
akiwemo Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wakitaka wawajibishwe kwa kuondolewa
kwenye nyadhifa zao kutokana na kushindwa kuchukua hatua wakati
operesheni hizo zikipoteza maisha ya watu na mifugo.
Mbali na Pinda, wamo pia Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani),
Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), David Mathayo David (Mifugo na
Uvuvi) na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa).
Dalili mbaya kwa viongozi hao zilianza kuonekana jana asubuhi baada
ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kutangaza kuwa amekubali hoja za
wabunge wawili waliotaka shughuli za Bunge ziahirishwe ili kujadili
jambo la dharura.
Alisema Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba (CCM) alitaka Bunge lijadili
kuhusu migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, huku
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), alitaka Bunge lijadili vitendo
vinavyofanywa na watendaji katika Operesheni Tokomeza Ujangili.
Lugola alidai watendaji wamekuwa wakiwaua kwa risasi ng’ombe
waliowakamata kwenye operesheni hiyo pamoja na kuwatesa wamiliki
wasiotoa fedha zinazohitajika.
Kutokana na hoja hizo, Makinda alitoa fursa kwa Waziri wa Maliasili
na Utalii, Khamis Kagasheki na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,
David Mathayo kuelezea Operesheni
Tokomeza Ujangili na migogoro kati ya
wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

