CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimeitaka tume ya katiba kuchukua
hatua dhidi ya watu wanaofanya vitendo vya udanganyifu kwa kuwasilisha
barua za maoni kwa tume hiyo. Akizungumza na waandishi wa habari huko
Dunga Mkoa wa kusini Unguja Katibu wa CCM wa mkoa huo, Zainab Shomari
alisema kumeanza kujitokeza vitendo vya udanganyifu wa watoaji maoni kwa
kutumia majina bandia kwa wawasilishaji.
“Kuna jina la Said Mwema limejitokeza katika barua na baada ya barua
hizo tume ilitaka kumjua huyo mtu anayeitwa Said Mwema lakini matokeo
yake hakuna aliyejitokeza, kwa hivyo sisi tuna mashaka na hao watu
wanaokwenda kupeleka maoni kwa njia ya barua tukiamini kuwa zinaandaliwa
na baadhi ya wanasiasa” alisema Zainab.
Akivitaja vitendo vyengine vinavyofanywa katika mchakato huo, Zainab
alisema ni pamoja na kuzomeazomea vilivyofanywa na vyama tofauti vya
siasa, kuwatumia wanafunzi kutoa maoni baada ya kupokea maelekezo kutoka
kwa walimu wao pamoja na baadhi ya wanasiasa kuwaongoza wafuasi wao na
kuwaelekeza maneno ya kwenda kutoa katika tume hiyo.
Katibu huyo alisema awali zoezi la utoaji maoni lilikuwa likiendelea
vizuri lakini katika siku za hivi karibuni kumeanza kujitokeza vitendo
vinavyoashiria uvunjifu wa amani ambapo baadhi ya watu wamekuwa
wakisimama kutoa maoni hali ya kuwa sio wakaazi wa maeneo husika.
“Kwa nyakati tofauti wananchi wa maeneo ya Mzuri na Mtende
wameshuhudia baadhi ya wazanzibari wa kutoka maeneo mengiwakifurika huko
kwa lengo la kutoa maoni mbele ya tume hiyo kinyume na taratibu za
nchi” aliwaambia waandishi wa habari.
Katibu huyo alisema kwamba baadhi ya wazanzibari hao bila ya
kigugumizi wala khofu “wakaanza kuandika mami ya barua za kughushi na
hatimae kuziwasilisha mbele ya tume ya jaji Warioba ili zikubaliwe na
kuyafanya ni miongoni mwa maoni yaliyotolewa na wananchi wa vijiji
hivyo”.
Akitoa ushuhuda wa matukio hayo Katibu huyo alisema Kizimkazi Dimbani
baada ya kutokea hayo Dk Salim Ahmed Salim alitoa karipio kali dhidi ya
wavunjaji wa sheria ambapo wananchi wa kijiji cha Bwejuu na vijiji
virani walikuwa wakishuhudia vitendo hivyo.
“Tume ya katiba ililazimika kusitisha zoezi hilo ili kutumia muda huo
kwa kutoa ufafanuzi kwa wananchi juu ya kitendo hicho cha kihuni na
atimae kuwataka waachane kabisa kuendelea kuvifanya kwa vile havina
hatima nzuri kwao na wala taifa” alisema Zainab.
Aidha alisema baadhi ya walimu katika kijiji cha Bwejuu wamejitokeza
baadhi ya walimu wa skuli za serikali wanaowashawishi wanafunzi wao
kwenda kutoa maoni kwa matakwa ya walimu hao. Chama hicho kimesema
kinaalaani vitendo hivyo vinavyokwenda kinyume na sheria pamoja na
kuitaka tume iwe macho na vitendo hivyo na wasisite kuchukua hatia za
kisheria dhidi ya wale wote ambao wana lengo la kuharibu zoezi hilo.
“CCM inatoa wito kwa wanachama na wapenda amani, utulivu na maendeleo
ya taifa letu wa maeneo yote ya mikoa ya Zanzibar kuwa macho na wale
wote wenye lengo la kuvuruga kwa makusudi zoezi hili, kwa kuwatolea
taarifa mbele ya vyombo vya dola, ili sheria ichukue mkondo wake didhi
yao” alisisitiza Zainab.
Via Zanzibar yetu.com
No comments:
Post a Comment