Alazwa Muhimbili, awaomba madaktari wasimdhuru
MKUU wa Upelelezi wa Kituo cha Polisi Kawe (OC CID), David
Mapunda, ametoa siri ya kutekwa, kupigwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Chama cha Madaktari, Dk. Steven Ulimboka.
OC CID huyo ambaye kwa sasa amelazwa katika Kitengo cha Mifupa cha
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Moi) alilazimika kutoboa siri ya kipigo
cha Dk. Ulimboka ili aweze kupata matibabu ya majeraha ya ajali ya
kugongwa na gari aliyoipata juzi.
Dk. Ulimboka alipookotwa na wasamaria wema katika msitu wa Pande na
kufikishwa katika kituo cha polisi Bunju, kilicho chini ya kituo cha
Kawe, OC CID huyo anadaiwa kutoa amri ya Dk. Ulimboka kukaa zaidi ya
saa tatu ili asipate matibabu ya haraka.
Vyanzo vyetu vya habari vililiambia gazeti hili kuwa mara baada ya
kugongwa na gari juzi, kigogo huyo wa polisi alijitahidi sana kukwepa
kwenda Muhimbili lakini alijikuta akiishia mikononi mwa madaktari wa
taasisi hiyo ya mifupa ya Moi, hivyo aliingiwa hofu ya kutotendewa haki
ya matibabu.
Kabla ya kufikishwa Muhimbili, askari huyo alikwenda katika Hospitali
ya Rufaa ya Lugalo na Aghakan, lakini alijikuta anatakiwa kufika Kitengo
cha Mifupa cha Moi, Muhimbili, ambako hadi sasa bado anaendelea na
matibabu.
Kwa mujibu wa habari hizo kutokana na hofu ya kususiwa na madaktari,
polisi huyo alilazimika kuwapigia magoti na kueleza mengi kuhusu kipigo
cha Dk. Ulimboka na kwamba yeye hahusiki na sakata hilo.
Mtoa habari wetu alisema kuwa OC CID huyo mara baada ya kufikishwa
hospitalini hapo akiwa na maumivu makali, alisema hahusiki na kipigo cha
Dk. Ulimboka na hata siku ya tukio hakuwepo.
Katika hali isiyo ya kawaida, kigogo huyo alijitetea huku akiwa na maumivu makali ya majereha aliyopata.
“Mimi sijahusika kabisa na kutekwa kwa Ulimboka. Jamani msinidhuru. Tena siku hiyo mimi sikuwepo,’ alikaririwa OC CID akisema.
Habari zaidi zinasema kuwa askari huyo aliendelea kueleza mengi na
hata alipotakiwa kuchomwa sindano, alionyesha woga na kuuliza anachomwa
sindano gani.
Ili kuhakikisha anatibiwa vizuri, kumekuwa na doria za kila mara ndani
na sehemu mbali mbali za wodi za MOI hali iliyowafanya madaktari na
wauguzi wa hospitali hiyo kulalamikia hali hiyo.
Mbali ya OC CID huyo kuingiwa na hofu ya kulipiziwa kisasi, hofu hiyo
pia imewakumba ndugu zake kwani hawana amani na matibabu ya ndugu yao.
Tanzania Daima Jumatano ilipofika katika hospitali Muhimbili,
ilishuhudia kuwapo kwa askari polisi wakilinda doria, huku OC CID akiwa
amelazwa chumba cha peke yake akiendelea kutibiwa.
Akizungumza na gazeti hili jana, mmoja wa madaktari wa Muhimbili
ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema Mapunda alifikishwa
hospitalini hapo juzi akiwa katika hali mbaya na mara baada ya
kufikishwa aliomba msamaha kwamba hakuhusika kumteka Dk. Ulimboka.
“Ni kweli jamaa alipokelewa lakini tulishangaa kwani alikuwa akiongea
kwa kuweweseka kwamba hajahusika na tukio la kumteka na kumtesa Dk.
Ulimboka na akawa anaomba tusimdhuru,” alisema daktari huyo.
Kwa mujibu wa daktari huyo, kilichowashangaza zaidi ni ulinzi mkali wa
polisi aliowekewa mgonjwa huyo huku kukiwa na watu wanaofuatilia kila
anayeingia katika wodi namba D aliyolazwa.
Afisa Uhusiano wa Moi, Jumaa Almasi, alisema mgonjwa huyo alifikishwa
hospitalini hapo wiki iliyopita akiwa amepata majeraha mwilini baada ya
kugongwa na gari.
Kuhusu mgonjwa huyo kumtaja Dk. Ulimboka, Almasi, alisema hawezi
kuzungumzia tukio hilo kwani hakuwepo wakati akifikishwa hospitalini
hapo.
Kwa Upande wake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles
Kenyela, alithibitisha kupata ajali kwa OC-CID Mapunda na kuongeza kuwa
ajali hiyo aliipata wakati akitekeleza majukumu yake.
Alisema hakuna uhusiano wowote wa tukio la kutekwa Ulimboka na ajali hiyo.
Tangu tukio la kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka serikali kupitia
maafisa wake wa usalama wamekuwa wakihusishwa kwa namna moja au
nyingine.
Kuhusishwa huko kwa serikali hususan jeshi la polisi kunafuatia
matukio mbalimbali ikiwa ni pamoja na afisa upelelezi kutoka kituo cha
Selanda Bridge katika eneo la Muhimbili, matamshi ya kutatanisha ya
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Suleiman Kova pamoja na
kukamatwa kwa mtu aliyedaiwa kuungama kanisani kuwa ndiye aliyemteka na
kumtesa Dk. Ulimboka.
Via Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment