EFM RADIO

EFM RADIO

HERICONY

Tangaza hapa

Tangaza hapa

TANGAZA NA BLOG YAKO HAPA

TANGAZA NA BLOG YAKO HAPA

Wednesday, July 4, 2012

Msangi, ANAYETUHUMIWA kumteka Dkt. Ulimboka azungumza

Picture
*Ni Kamanda Msangi anayeongoza Tume ya kuchunguza utekaji ulivyotokea
*Ujumbe wasambazwa kuwa ndiye alimpora simu ya mkononi na ‘wallet’
*Yeye asema amekatishwa tamaa, Professa Museru aeleza alichosikia

Askari anayetuhumiwa kumteka Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dkt. Stephen Ulimboka, Kamishna wa Polisi Msaidizi (ACP), Ahmed Msangi, amehojiwa na kuzungumzia kilichotokea kuhusiana na tuhuma kwamba aliambiwa arejeshe simu ya mkononi na pochi ya Dkt. Ulimboka.

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI, ACP Msangi alikiri kwenda katika wodi ya wagonjwa mahututi katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa nia ya kumhoji Dkt. Ulimboka, ila akaeleza mshangao wake kutokana na habari zilizochapishwa mwishoni mwa wiki, kuwa aliambiwa arejeshe pochi na simu ya Dkt. Ulimboka kwa maana kuwa alivipora walipomteka.

Vyombo vya habari mwishoni mwa wiki vilichapisha taarifa bila kutaja jina la askari anayetuhumiwa, lakini pia ukawa unasambazwa ujumbe mfupi kupitia simu za mkononi ambao ulisema hivi:

“Kamanda Msangi aliyemkamata na kumtesa Dkt. Ulimboka, yuko katika jopo la kuchunguza nini kilimtokea Dkt. Ulimboka. Alipofika kumhoji Dkt. Ulimboka alimwambia ‘Nirudishie simu na wallet yangu’. Kamanda Msangi taratibu akaondoka wodini kichwa chini. Kama wewe ni mpenda haki na unapinga ujinga na dhuluma, watumie ujumbe huu watu wengi kadri uwezavyo ili wamjue dhalimu aliyeongoza unyama huu,” ulisema ujumbe huo unaosambazwa kupitia simu za mkononi.

Tume ya Jeshi la Polisi iliyoundwa kuchunguza tukio la Dkt. Ulimboka kutekwa nyara, kwa mujibu wa Kamanda Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, inaongozwa na Kamanda Msangi.
 
Kamanda Msangi azungumza Jamhuri: Afande umetangazwa kuongoza hii Tume ya Polisi kuchunguza suala la Dkt. Ulimboka, lakini taarifa zilisosambaa zinaonyesha Ulimboka alikwambia umerejeshee simu na wallet yake. Unalizungumziaje hili?

Kamanda Msangi:
Hata mimi nimesikia hizi taarifa, na zimenisikitisha mno. Naamini taarifa hizi zina malengo ya ziada. Si kweli kwamba nilishiriki kumteka Dkt. Ulimboka na wala sijawahi kuwa na wazo hilo.

Jamhuri: Ikiwa hukushiriki kumteka iweje wodini akwambie nirudishie simu yangu?

Msangi: Kwanza ifahamike mimi huyu Dkt. Ulimboka na mwenzake Dkt. Deo nimewafahamu siku nyingi sana. Kwa maana hiyo ni mtu anayenifahamu vizuri tu. Kuna upotoshaji wa makusudi umefanywa ambao mimi nadhani una msukumo wa kisiasa.
Alichosema Dkt. Ulimboka nilipozungumza naye, ni kwamba simu moja ilidondoka, nyingine wale watu waliomteka wameichukua pamoja na wallet yake. Hivyo alikuwa ananitajia vitu vilivyopotea. Nilipomuuliza iwapo anakumbuka namba ya simu, aliniambia nikamuulize Dk. Deo. Sasa nashangaa mtu aliyepenyeza uongo huu kwamba alisema mimi ndiye niliyempora hivyo vitu… sielewi ni nani na ana malengo gani.

Jamhuri: Haya unayasema wewe, hivi unadhani jamii itakuamini kwa kauli hizi, haitaonekana unajitetea tu?

Msangi: Wakati anazungumza maneno haya, alikuwapo Profesa Museru ambaye ni Mkurugenzi wa MOI. Sina cha kuficha kamuulize tu, atakwambia alichosema Dkt. Ulimboka. Yupo pia Dkt. Deo, huyu ananifahamu na Dkt. Ulimboka anasema walikuwa wote wakati anatekwa. Dk. Deo ananifahamu, akaulizwe iwapo mimi ndiye niliyemteka Dk. Ulimboka.

Jamhuri: Tuhuma hizi zilianza kusambaa mapema tu Ijumaa. Je, wewe hukuwa na hofu kwenda pale MOI kumhoji Dkt. Ulimboka?

Msangi: Ndugu yangu, nchi hii ina askari wengi mno. Hivi mimi kwa akili ya kawaida naweza kushiriki kumteka Dkt. Ulimboka kisha nikaenda wodini kumhoji? Hata katika akili ya kawaida ya binadamu hilo haliwezekani.

Jamhuri:
Hizi tuhuma zilizoelekezwa kwako ni nzito. Wewe ndiye uliyeteuliwa kuongoza Tume ya Uchunguzi wa tatizo hili. Je, unadhani uchunguzi utakaofanya utaaminiwa na wananchi ukitoa ripoti?

Msangi: Mimi ninachokuhakikishia sikushiriki kumteka na si kweli kwa kila hali. Mambo kama haya yanakatisha tamaa. Kama tunaanza kuzushiana uongo kwa kiwango hiki, nchi hii sijui inaelekea wapi! Kimsingi imenikatisha tamaa mno. Wapo wanaosema nijiuzulu katika Tume hii lakini mimi nasema wakubwa wangu wamenipa kazi hii na watakaloamua nitalipokea. Hivi wewe gazeti lako likituhumiwa unaacha kuendelea kutafuta habari? Nitaendelea kufanya kazi hii kama nilivyoapa siku nilipohitimu mafunzo kwamba nitalitumikia taifa kwa uadilifu na uaminifu wa hali ya juu katika kiapo changu cha utii. Na hilo ndilo nitakaloendelea kufanya. Watu wanapenda kuharibiana maisha tu.


Profesa Museru asema alichokisikia Mkurugenzi wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru, akizungumza na JAMHURI kuhusiana na sakata kwamba Dk. Ulimboka, alimweleza Kamanda Msangi arejeshe simu na wallet yake.

Jamhuri:
Profesa nimezungumza na Kamanda Msangi juu ya tuhuma zinazomkabili kuwa aliambiwa na Dk. Ulimboka amrejeshee simu na wallet yake, na akakutaja wewe kuwa ulikuwapo wakati wa mazungumzo hayo. Wewe nini ulichokisikia kuhusiana na tuhuma hizi.

Profesa Museru:
Mimi ndiye niliyempeleka pale wodini. Ni bwana mzuri tu. Nilimu-introduce (nilimtambulisha), akaanza mahojiano. Mimi hilo sikulisikia kwamba ameambiwa arejeshe simu na wallet, hilo sikulisikia.

Jamhuri: Kuna habari kuwa Kamanda Msangi baada ya kuambiwa kauli hiyo alitoweka wodini bila kuaga akikwepa kipigo kama ilivyomtokea askari mwenzake siku mbili kabla. Je, unalizungumziaje hilo profesa?

Profesa Museru: Nini? Kwamba alikimbia? Jamani nchi hii inakwenda pabaya. Mimi nilimsindikiza hadi nje ya wodi akapanda gari lake na kurejea ofisini kwake, sasa hilo la kukimbia limetokea wapi? Jamani ehee, mimi niseme katika hali kama hii sintofahamu zipo nyingi. Ni vyema kuchuja taarifa tunazozipata.


Daktari asisitiza polisi wanahusika


Gazeti la JAMHURI lilichukua jukumu la kumtafuta mmoja wa viongozi wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, ambaye kwa sababu za kiusalama alikataa jina lake lisitajwe gazetini, lakini yeye alisisitiza kuwa polisi wanahusika na utekaji huo kwa asilimia 100.

“Hivi unategemea leo Kamanda Msangi kwa akili ya kawaida ya binadamu anaweza akakiri kuwa alishiriki kumteka? Taarifa tulizonazo ni kwamba polisi ndiyo waliomteka Dk. Ulimboka na kumfanyia unyama huu.

“Ndiyo maana tunasema polisi tayari wanatuhumiwa hivyo hawana haki ya kuchunguza suala hili. Tunataka ateuliwe Jaji, na Tume iwe na wajumbe huru wasiofungamana na chama, taasisi au siasa za nchi hii, wachunguze kwa kina na kutoa taarifa huru,” alisema Daktari huyo.

Alisema mbinu iliyotumika kumtesa Dkt. Ulimboka hutumiwa na majasusi wenye mafunzo ya hali ya juu, ambayo hata majambazi wa kawaida hawawezi kuzifahamu.

“Unapomg’oa mtu kucha au jino bila kumpiga ganzi, unashtua mishipa ya fahamu kumfanya anayeteswa afahamu kuwa kinachofuatia dhahiri ni kifo, na hivyo kulazimika kusema ukweli wote anaojua juu ya suala analohojiwa. Mtu akishang’olewa jino au kucha na asiseme chochote, basi unajua fika kuwa hakuna anachokifahamu zaidi ya alichokisema.

“Hii inatokana na nini? Hicho kinatokana na ukweli kwamba baada ya kung’olewa kimojawapo kati ya hivyo, kinachofuata ni kupoteza fahamu. Sekundi chache kabla ya kupoteza fahamu nati za mishipa ya fahamu huwa zinafunguka na kusema kila kilicho cha kweli bila wewe unayeteswa kujua. Ndiyo maana nasema vyombo vya dola ndivyo vilivyohusika. Haya ni mateso ya kitaalamu,” alisema daktari huyo.

Rais wa Chama cha Madaktri Tanzania, Dkt. Namala Mkopi, alipopigiwa simu na JAMHURI kueleza chochote anachokifahamu katika sakata hili, alipokea simu akasikiliza kisha akakata bila kujibu na hata alipopigiwa simu tena hakutaka kuipokea tena.

Dk. Ulimboka apelekwa nje kwa matibabu Madaktari inaelezwa kuwa wameamua kumpeleka Dk. Ulimboka katika matibabu nchini India, ingawa kwa sababu walizosema ni za kiusalama hawakutaka kutaja ni hospitali gani aliyopelekwa.
Jumanne wiki iliyopita, Dkt. Ulimboka alitekwa na watu wasiofahamika hadi sasa na kupigwa, akang’olewa meno mawili na kucha mbili, kisha akatupwa katika msikiti wa Mabwepande baada ya kuwa ameteswa kupita kiasi.
Dkt. Ulimboka baada ya kuokotwa na wasamaria wema, alikaririwa na Radio Clouds akisema kuwa walipokuwa Kinondoni ndipo alipotekwa usiku wa saa 5:30.

"Mara, katikati ya maongezi tukaona mtu anaongea na simu. Ghafla tukiwa tunasema tuagane, wakaja watu kama watano hivi na bunduki, wakasema wewe na yule bwana mko free (huru), tunakuchukua wewe (Dkt. Ulimboka)," alieleza na kuongeza.
"Sijakaa sawa, nikaona nimeshaburutwa nikaanguka kwenye lami, wakaniinua na kuniingiza kwenye gari nyeusi, lakini ilikuwa haina namba."

Wananchi wataka uchunguzi huru Baadhi ya wananchi waliozungumza na JAMHURI huku wakionyesha hofu ya kutaja majina yao, walilituhumu Jeshi la Polisi kuwa linahusika moja kwa moja na tukio hili hivyo wakuu wa jeshi hilo wawajibike kuhakikisha ukweli unapatikana.

“Ndugu yangu nawahurumia nyie wenye kutafuta habari hizi. Mnafanya kazi ya hatari. Tutazidi kuwaombea tu, muishi milele na Mungu awalinde. Hivi leo kwa mfano unaweza kwenda kumhoji Msangi kuwa unatuhumiwa kumteka Dkt. Ulimboka? Ukitoka hapo anatuma vijana wake nao wanakuteka na wewe pia.

“Naamini polisi walihusika kwa kiwango kikubwa na hivyo hawapaswi kushiriki uchunguzi huu. Hawa wanapaswa kupanda kizimbani kujitetea hivyo ni makosa kushiriki uchunguzi wao,” alisema Mkazi wa Dar es Salaam.

Mwananchi mwingine alisema chimbuko la mgogoro wa madaktari liko wazi. “Hawa wanadai mishahara mizuri na marupurupu sawa na wanavyopata wabunge wasiofanya kazi yoyote. Leo unadhani serikali inaona imeshikwa pabaya itawaacha waendelee kutamba tu? Thubutu. Kimsingi polisi wametumiwa. Hao waliowatumia ndiyo tunaotaka uchunguzi huru utueleze ni kina nani na kwa nia ipi,” alisema Mkazi wa Arusha kwa njia ya simu.

Hadi sasa madaktari katika hospitali za umma wamegoma kuendelea na kazi kutokana na mgogoro wa malipo kati yao na serikali, na hivi karibuni mgogoro huo umeshika kasi baada ya Dkt. Ulimboka kutekwa na kuumizwa vibaya.
via gazeti la Jamhuri Jumanne, Julai 03, 2012 - JamhuriMedia.co.tz

No comments:

Post a Comment

HABARI MBALIMBALI

‘Dk. Cheni’ ‘Sharo Milionea ‘Thea’ African Women AGNESS MASOGANGE AK CLASSIC COSMETICS ALI KIBA Amanda Poshy Ant ANT LULU Ashley Toto Aunt Ezekiel Aunty Ezekiel AUNTY LULU Azam Fc Baby Madaha BAHATI BUKUKU Barnaba BATULI BBA Beauty of the day Belle 9 BI KIDUDE BIBI BOMBA Big Brother Big Brother Africa Bill Gates BINTI KIZIWI BOB JUNIOR Bodi ya Filamu Bongo Movie Bongo Movies CCM CHADEMA Chombezo Christina Shusho Chuchu hans. Clouds Media Group Club Bilicanas DAR LIVE DAVINA Dayna Nyange Diamond Dida Diva Loveness Love Dj Ommy Crazy wa Maisha Club DOGO JANJA DOKI DR.CHENI DSTV Dude Dully Sykes EBSS 2013 Elizabeth Michael Epiq Bongo Star Search (EBSS) ESHA BUHETI Ester Bulaya Feza Kessy FIESTA 2014 Flaviana Matata FLORA MBASHA FLORA MVUNGI Francis Cheka GARDNER GLOAL PUBLISHERS GLOBAL TV ONLINE H. BABA Halima Mdee HAMISA Happy birthday Hemedi Hemedy Suleiman HOTUBA YA RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE Hoyce Temu Huddah Monroe HUSINA IRENE PAUL Irene Uyoya ISABELLA J film 4 life Jack Chuz JACK PATRICK Jacob Steven ‘JB’ Jacqueline Dustan JACQUELINE WOLPER Jaji Khamis 'Kashi' Jay Dee JENNIFER KYAKA (ODAMA) JIDE JINI KABULA JK JO Johari Jokate Mwigelo ‘Kidot’. JOTI Joyce Kiria Joyce Kiwia JUX K-LYNN KADINDA kaja Kajala Masanja Kapotive Star Singers KATUNI Kemmy Kero Zetu KHADIJA OMAR KOPA KIKWETUKWETU KILI MUSIC AWARDS KOLETA Lady Jay Dee Lady Jaydee Lake Oil LAVEDA Linah Sanga Linex Lisa Jensen Loveness Diva Lucy Francis Komba Lulu M2 The P MABILIONEA Madam Rita MADELA Magazeti Mahusiano Maimartha Jesse MAINDA MAISHA Makala Malkia Elizabeth MAMTEI MANDELA MARIAM ISMAIL Masanja Mkandamizaji Mashindano ya Miss Tanzania Matangazo Matonya MaxMalipo MAYA MELLIS EDWARD MENINAH MGOSI MKOLONI Mh Halima Mdee mic Michezo MILLEN HAPPINESS MAGESE MISS CHANG'OMBE MISS DAR CITY CENTER Miss East Africa MISS REDD'S IRINGA 2013 MISS TANGA 2013. MISS TANZANIA 2014 Miss Tanzania mwaka 2011 MISS TEMEKE 2014 MISS USTAWI MISS UTALII TANZANIA 2012/13 Miss vyuo vikuu 2013 MKALA MREMBO HUDDAH Mrisho Mpoto Mrisho Ngassa MSHINDI WA REDD'S MISS LAKE ZONE 2013 NI LUCY CHARLES. MSHINDI WA TAJI LA REDDS MISS KANDA YA KATI 2013 Mtitu muziki Mwana FA MWANAMKE BORA WA MWAKA 2013/14 Mzee Majuto Nancy Sumari Nani Mtani Jembe? NAPE Nassoro ‘Nora’ Natasha Nay wa Mitego Necta Nelly Kamwelu NEY WA MITEGO Nisha NSSF;Zantel Nyamwela NYimbo Nyota yako OBAMA TANZANIA OMMY DIMPOZ P FUNK PAM D Peniel Mgilwa ‘Penny’ PETIT MAN Profesa Jay Q - CHILA Q Boy Q Chilla QUEEN DARLEEN RACHEL NDAUKA RAIS KIKWETE Rais Kikwete. Rasimu Ya Katiba TZ Ray Ray C Redd’s Miss IFM REDD'S MISS KAGERA 2013 REDD'S MISS TZ REDDS MISS TANZANIA 2014 Redds Miss wa Mikoa REHEMA FABIAN RICHIE RICHIE Rihanna ROSE MUHANDO Rose Ndauka Ruge Mutahaba. SABASABA 2013 Saida Karoli Saikolojia Sajeti SAJUKI Sandra SHAA Shamsa Ford Sheikh Ponda Shilole Sintah Siwema Skin Tricks Snura Mushi Spika Makinda staa Staa Wetu Stella Mwangi STYLE ZA NYWELE Taifa Stars Tamasha la matumaini TAMASHA LA SERENGETI FIESTA 2013 Tangazo TANZANIA TEGO TENGENEZA WEBSITE NA BLOG TID Tundaman Tupo wangapi? TUZO ZA MWANAMKE BORA WA MWAKA 2013/14 Twanga Pepeta USA PAGEANT 2014‏ VAI Wastara WEMA WEMA SEPETU Yanga Yanga Bingwa 2013 YOUNG D Yvonne Cherry ‘Monalisa’ Z Anton. Zari Zito kabwe

Translate