WATU wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wameuawa na polisi
mkoani Arusha wakati wakirushiana risasi huku wengine wanne wakifanikiwa
kutoroka.
Tukio hilo limetokea juzi saa 2:15 usiku kwenye Kijiji cha Makisoro,
Kata ya Akheri wilayani Arumeru, ambapo baada ya kuuawa majambazi hao
ambao majina yao hayajafahamika, polisi walichukua bunduki waliyokuwa
wakiitumia aina ya Mark IV yenye namba 5903629B ikiwa na risasi tisa.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas, aliwaeleza waandishi
wa habari jana kuwa miili ya marehemu hao ambao wote ni wanaume
imehifadhiwa kwenye hospitali ya mkoa ya Mount Meru.
Akielezea tukio hilo, Kamnda Sabas alisema kuwa polisi wakiwa kwenye
doria ya kawaida walipita eneo hilo ambapo waliwaona watu hao na
kuwatilia shaka hivyo kuamua kuwahoji ndipo ghalfa watu hao wakaanza
kuwarushia polisi risasi.
Alisema kuwa polisi nao waliamua kujibu ndipo watu hao wawili wakauawa
huku wengine wanne wakifanikiwa kukimbia ambapo uchunguzi wa kuwabaini
majina ya waliokufa na waliokimbia unaendelea.
Katika hatua nyingine jeshi hilo limefanikiwa kukamata watu 17
wakiwemo watano wanaotuhumiwa kujihusiasha na ujambazi wa kutumia
silaha.
Habari Grace Macha, Arusha
No comments:
Post a Comment