HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA M.
KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWA WANANCHI
KUHAMASISHA SENSA YA WATU NA MAKAZI, TAREHE 25 AGOSTI, 2012
Ndugu wananchi;
Imekuwa ni mazoea yetu kuwa Rais huzungumza na taifa kila mwisho wa mwezi. Lakini, leo nazungumza nanyi siku saba kabla ya mwisho wa mwezi kwa sababu maalum. Sababu yenyewe si nyingine bali ni Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika kwa siku saba kuanzia kesho Jumapili tarehe 26 Agosti, 2012. Shabaha yangu ni kutaka kuwakumbusha Watanzania wenzangu wote kuhusu wajibu wao wa kujitokeza kuhesabiwa siku hizo. Naomba kila mmoja wetu ahakikishe kuwa anakuwepo kuhesabiwa na kujibu maswali yote yatakayoulizwa na makarani wa sensa kwa ufasaha.
Ndugu wananchi;
Katika historia ya nchi yetu, Sensa ya mwaka huu itakuwa ni ya tano tangu Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari, 1964 na kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Aprili, 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988 na 2002. Kumbukumbu zinaonesha kuwa kwa upande wa Tanzania Bara wakati wa ukoloni zilifanyika Sensa mwaka 1910, 1931, 1948 na 1957. Kwa upande wa Zanzibar wakati wa ukoloni na utawala wa Sultan kulifanyika Sensa mara moja mwaka 1958.
Ndugu Wananchi;
Kama ilivyokuwa kwa Sensa zilizotangulia, madhumuni makubwa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ni kujua idadi ya watu, mahali walipo, jinsia zao, umri wao, elimu, shughuli wazifanyazo, vipato vyao, upatikanaji wa huduma mbalimbali pamoja na makazi. Taarifa hizi hutumiwa na Serikali kupanga mipango ya maendeleo, kutengeneza programu mbalimbali na kubuni miradi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. Aidha, huisaidia Serikali kupanga na kupeleka huduma za kiuchumi na kijamii kwa wananchi kwa kuzingatia mahitaji halisi ya maeneo yao wanayoishi kwa mujibu wa idadi yao na mgawanyiko wao kijinsia, kiumri na huduma zinazohitajika. Hivyo basi, idadi halisi isipojulikana kuna hatari ya wananchi kukosa huduma wanazohitaji kwa kiwango kinachostahili. Vilevile, takwimu hizi hutumiwa na Serikali katika kufikia uamuzi wa kugawa majimbo ya uchaguzi na maeneo ya utawala kama vile mikoa, wilaya, kata, vijiji na vitongoji vipya.
Ndugu wananchi;
Pamoja na umuhimu huo wa jumla wa Sensa kwa maendeleo ya nchi yetu, Sensa ya mwaka 2012 ina umuhimu wa aina yake. Taarifa zake zitatumika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa Dira za Taifa za Maendeleo za Tanzania Bara na Zanzibar; Mkakati wa Kukuza na Kupunguza Umaskini Tanzania Bara (MKUKUTA II); Mkakati wa Kupunguza Umaskini Zanzibar (MKUZA II); na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2011/12 – 2015/16. Vilevile taarifa zitakazopatikana zitatumika kupima maendeleo ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia (Millenium Development Goals) yaliyowekwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2000. Kama tujuavyo, itakapofika mwaka 2015 ndicho kilele cha utekelezaji wa Malengo hayo hivyo kujua hatua tuliyofikia sasa itasaidia kujipanga vizuri katika miaka mitatu iliyosalia.
Ndugu Wananchi;
Pamoja na faida hizo, taarifa za Sensa hii zitasaidia kufanikisha zoezi linaloendelea sasa, la kuwapatia Watanzania vitambulisho vya taifa. Baadhi ya maswali yatakayoulizwa kwenye Sensa ya Watu na Makazi yatasaidia katika kuhakiki maombi ya vitambulisho vya taifa. Bila ya shaka sote tunatambua vyema manufaa ya vitambulisho vya taifa, hivyo basi ndugu yangu, shiriki zoezi la sensa ili kuirahisishia Serikali kazi ya utoaji wa vitambulisho kwa raia wake.
Ndugu wananchi;
No comments:
Post a Comment