Takwimu zinaonyesha kuwa kwa mwaka 2011 zaidi ya watu milioni 34 ulimwenguni wanaishi na maambukizi ya Virusi vya ugonjwa wa Ukimwi (VVU) kati ya hao milioni 30.7 watu wazima, milioni 16.7 wanawake na milioni 3.4 watoto wenye umri wa chini ya miaka 15.
Hayo yamesemwa jana na Mwakilishi
wa Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Kupambana na Ugonjwa wa Ukimwi
(UNAIDS) Dkt. Raul de Melo Cabral wakati akiongea na wake wa wakuu wa
nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) waliohudhuria mkutano wa kuzuia
maambukizi ya virusi vya Ugonjwa wa Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa
mtoto kwa maendeleo ya kanda unaofanyika Maputo nchini Msumbiji.
Dkt. Cabral alisema kuwa ugonjwa wa Ukimwi utaendelea kuwa changamoto kwa nchi zote na kila mtu anatakiwa kupambana nao ndiyo maana katika Azimio la Kisiasa lililofanyika mjini New York mwaka 2011 wakuu wa nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) wakiwemo wa SADC walipitisha malengo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua zaidi katika kupambana na ugonjwa huo.
“Walikubaliana kuwa ifikapo mwaka 2015 wawe wamepunguza nusu ya maambukizi ya ugonjwa huo katika nchi zao, kupunguza maambukizi mapya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kutoa matibabu kwa watu milioni 15 katika nchi zote wanachama wa umoja huo wanaoishi na VVU na kuongeza bajeti katika masuala yanayohusiana na afya”, Alisema.
Akichangia
mada katika mkutano huo Mke wa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi
ya wanawake na Maendeleo (WAMA) Mama Salma Kikwete alisema kuwa ni
jambo jema kwa wake wa viongozi wa SADC kuwa na mfumo mzuri wa utendaji
kazi ambao utawawezesha kufanya mambo yatakayokuwa na tija katika kanda na kuweza kuwasaidia wanawake na watoto ambao kwa kiasi kikubwa wameachwa nyuma kimaendeleo.
“Sisi kama wanachama tunatakiwa kutengeneza mpango mkakati na kuona jinsi gani unaweza kujitoa ili kuweza kutimiza malengo tuliyojiwekea ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yanapungua au kutokuwepo kabisa katika jamii inayotuzunguka”, alisema Mama Kikwete.
Aliendelea
kusema kuwa pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kuwasaidia
rasilimali ambazo wanazifanyia kazi kila siku wao pia wanajukumu kubwa
la kuhakikisha kuwa wanachangia kwa kiasi kikubwa ili waweze kutimiza malengo waliyojiwekea.
Kwa upande wake Mke wa Rais wa Zambia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa wake wa Marais wa Afrika wa Kupambana na Ugonjwa wa Ukimwi (OAFLA) Dkt. Christine Kaseba Sata alisema kuwa hivi
sasa nchi za SADC zinafanya jitihada kubwa ya kupunguza maambukizi ya
ugonjwa huo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (MTCT) baada ya kugundua
kuwa ugonjwa huo ni wa hatari si tu kwa watu wanaoishi na ugonjwa huo bali hata kwa watoto wanaoupata kutoka kwa mama zao.
Dkt. Sata alisema kuwa Ugonjwa wa Ukimwi unatishia maisha ya watu kwa kizazi kilichopo na kijacho kwani watoto wengi wanaozaliwa kama watakuwa na maambukizi hawataweza kuishi muda mrefu, ugonjwa huo unaharibu familia, kupunguza uzalishaji na uchumi katika ngazi ya familia na kutokuwa na kizazi kisichokuwa na urithi kwa kizazi kijacho.
“Licha ya kupambana na ugonjwa wa Ukimwi changamoto nyingine tunayokabiliana nayo ni
ya kuenea kwa kasi kwa ugonjwa wa shingo ya kansa ya kizazi na matiti
kwa wanawake wengi katika nchi wanachama wa Umoja wa SADC, wanawake hawa wanakufa kwa ugonjwa ambao unaweza kuzuilika na kutibika kama mgonjwa atapata matibabu mapema” , Dkt.Banda alisema,
Aliendelea
kusema kuwa wanawake wengi wanakufa kwa kukosa uelewa kuhusiana na
ugonjwa huo , kutofanyiwa uchunguzi na kupata huduma za matibabu mapema na kuwashauri wake hao wa viongozi kufanya kazi kwa ukaribu na Serikali ya nchi zao jambo ambalo litawafanya watu wengi zaidi kuwa na ufahamu kuhusiana na ugonjwa huo.
Mkutano huo wa siku mbili wenye kaulimbiu isemayo kuondoa maambukizi ya Ugonjwa wa ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto inawezekana unahudhuriwa na wake mbalimbali wa wakuu wa nchi wanachama wa SADC akiwemo mke wa Rais Mama Salma Kikwete
No comments:
Post a Comment