SUALA la utekaji nyara wa Dk. Steven Ulimboka lilikuwa limepoa lakini msanii wa Bongo Flava, Kalama Masoud 'Kalapina' ameliibua upya baada ya kutangaza atatengeneza filamu ya tukio hilo. Kalapina, ambaye anaongeza orodha ya wasanii wa Bongo Flava wanaojitosa kwenye fani hiyo, alidai kuwa filamu hiyo, ambayo ataanza kuiandaa hivi karibuni, itazungumzia maisha yake tangu akiwa shuleni.
Niko kwenye maandalizi ya filamu inayolenga kuonyesha maisha halisi ya Dk.Ulimboka, lengo ni kuwafanya Watanzania waelewe nini kilimkuta na kwanini ilikuwa hivyo, alisema Kalapina. Alisema licha ya tukio la Ulimboka kuwasikitisha watu wengi amejipanga kukabiliana na hali yoyote itakayomkuta kwa kuwa anajiamini.Wala sijali kama kuna atakayefikiria kuniua baada ya kufanya filamu hii wala sihofii kwa kuwa wote tutakufa,kama ngumi nitapigana yaani simwogopi mtu yeyote, alisema. Dk. Ulimboka alivuma baada ya kuongoza mgomo mkubwa wa madaktari kupitia Jumuiya ya Madaktari na kusababisha mvutano mkubwa na Serikali.
Hata hivyo, suala lake lilichukua sura mpya baada ya kutekwa nyara Julai 16, mwaka huu maeneo ya Leaders' Club jijini Dar es Salaam na kupigwa na watu wasiojulikana waliokuwa wakimshinikiza aeleze nani wanaomfadhili katika harakati zake za kuongoza mgomo. Baada ya kipigo hicho kikali, alitupwa katika msitu wa Mabwepande na kuokolewa na wasamaria mwema waliompeleka kwenye Kituo cha Polisi cha Bunju kabla ya kukimbizwa Muhimbili.
Hata hivyo, baada ya kulazwa hospitalini hapo, alipelekwa kwa matibabu zaidi nchini Afrika Kusini na baada ya kupona amerejea nchini. Tangu amerudi, Dk. Ulimboka amekuwa kimya mapumzikoni na suala na kitendo cha Kalapina kuibua filamu hiyo kinaweza kuzua mjadala tena wa suala hilo ambalo katika siku za karibuni lilikuwa limepoa.
No comments:
Post a Comment