Chanzo cha habari Tanzania Daima(05/09/2012)
ASKARI polisi aliyefyatu bomu lililomlipua na kumuua kinyama
mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, David
Mwangosi (40), amejulikana.
Tayari mazishi ya masalia ya mwili wa Mwangosi yamefanyika jana katika
Kijiji cha Busoka, Kata ya Itete, Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya, huku
ndugu, waandishi wa habari, wachungaji na wananchi wengine wakililaumu
Jeshi la Polisi kwa mauaji hayo, na kwa kushindwa kuwachukulia hatua
askari polisi waliosababisha kifo hicho na jina baya la jeshi hilo.
Picha zilizopigwa kwenye tukio la mauaji hayo, zinaonyesha askari
wakiwa wamemzingira na kumpiga Mwangosi, baadhi yao wakiwa na virungu,
na wengine bastola. Mmoja miongoni mwao, ameshikilia bunduki na
kuielekeza tumboni.
Vile vile, baadhi ya askari wamemtaja mwenzao aliyemlipua Mwangosi,
wakataja na mahali anakoishi mjini Iringa. Hata hivyo, hadi tunakwenda
mitamboni, polisi ilikuwa haijasema wazi kama imemtia mbaroni yeye na
wenzake, huku wizara na jeshi hilo zikiunda tume za kuchunguza “chanzo”
cha tukio hilo!
Baadhi ya askari waliokuwepo siku ya tukio, walilieleza gazeti hili
jana kwa sharti la kutotaja majina yao kwamba askari aliyemlipua
Mwangosi na kumuua papo hapo yuko chini ya ulinzi tangu siku ya tukio
pamoja na askari wengine walioonekana wakimpiga mwandishi huyo.
Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Michael Kamhanda, alipoulizwa kuhusu
taarifa hiyo, alisema hana taarifa za askari yeyote kushikiliwa na
kuhojiwa kwa tukio hilo.
Kutoka mazikoni, habari zinasema kuwa haikuwa kazi ndogo kuzuia vilio
na simanzi zilizoonyeshwa na umati mkubwa wa waombolezaji waliofika
kushuhudia mwili wa marehemu Mwangosi ulioharibiwa vibaya ukionyeshwa
baada ya Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Usharika
wa Busoka, Mathayo Mwantemanie kuongoza ibada ya mazishi.
Kifo cha mwandishi huyo ambacho kimevuta hisia za wananchi wengi ndani
na nje ya nchi, hususani wakazi wa Wilaya ya Rungwe, kilimgusa kila
mmoja akiwemo Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais asiye na
wizara maalum, Profesa Mark Mwandosya na mkewe, Lucy Mwandosya waliofika
nyumbani kwa marehemu.
Profesa Mwandosya alieleza jinsi msiba wa Mwangosi ulivyomgusa,
kumuumiza moyo na kumfanya ashindwe kujizuia kutoa machozi kwani tayari
alishapoteza wazazi wake wote wawili miaka michache iliyopita.
“Ni vigumu sana kwangu kuzungumzia hali hii, Mwangosi ameniuma sana,
nimezunguka naye sana, nimefanya naye kazi kwa karibu sana, nimepotelewa
na kijana wangu, mtoto wangu, mwenzangu katika kazi, kila nilipokuwa
naye alinipiga sana maswali na mengi yalikuwa ya msingi,” alisema
Profesa Mwandosya.
Kwa upande wake, Dk. Slaa ambaye alikuwa kwenye msafara wa kusafirisha
mwili wa marehemu, alieleza mazingira ya kifo hicho na kusema msiba
hauna itikadi, dini wala rangi, na kubeza kauli za ubaguzi dhidi ya
msiba wa mwanahabari huyo.
Alisema CHADEMA itahakikisha haki ya Mwangosi haipotei na kuongeza
kuwa binadamu si kuku, kwani damu yake lazima ipiganiwe kwa haki na
kueleza jinsi chama hicho kinavyoshtushwa na vitendo vinavyofanywa na
serikali dhidi ya vyombo vya habari, hususani kulifungia gazeti la
MwanaHALISI na sasa wameamua kupoteza maisha ya mwanahabari huyo.
Naye Mchungaji wa Kanisa la Kilutheri, Dk. Steven Kimondo na Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Tumaini Idara ya Thiolojia, aliuliza umati huo baada
ya kusema kuwa Jeshi la Polisi linahusika na mauaji ya Mwangosi.
“Akili yangu inakataa kusema uongo kuwa Jeshi la Polisi halihusiki na
tukio la kifo hiki, vitendo hivi vya mauaji ya raia wasiokuwa na hatia
vinajenga chuki kwa wananchi dhidi ya serikali yao na kwamba lazima
uchunguzi ueleze ukweli kuwa marehemu hajafa kifo cha Mungu isipokuwa
binadamu wamehusika,” alisema Dk. Kimondo.
Dk. Slaa alitoa ubani wa sh milioni 2, Mbeya Press Club (sh 700,000),
Iringa Press Club (sh 1,750,000), MISA-Tan (sh 500,000), huku Profesa
Mwandosya akiahidi kumsomesha mtoto mkubwa wa marehemu ambaye yupo
kidato cha nne na wadogo zake, na alitoa ubani wa sh 500,000.
Waziri Nchimbi aunda tume huru
Katika hatua nyingine, serikali imeunda tume huru ya watu watano wa
kada tofauti akiwemo mtaalamu wa milipuko kuchunguza mauaji ya Mwangosi.
Licha ya kuwepo kwa tume nyingine iliyoundwa na Jeshi la Polisi chini
ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema, tume ya serikali
itafanya kazi kwa siku 30 na imepewa hadidu sita za rejea.
Mwangosi aliuawa Septemba 2 mwaka huu kwa kitu kinachoaminika kuwa ni
bomu lililoelekezwa kwake na askari polisi waliokuwa wakiwadhibiti
wafuasi wa CHADEMA waliokuwa kwenye ufunguzi wa tawi katika Kijiji cha
Nyololo wilayani Mufindi, mkoani Iringa.
Akitangaza kuundwa kwa tume hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Dk. Emmanuel Nchimbi, aliwaeleza waandishi wa habari aliokutana nao
ofisini kwake jana kwamba hakuna askari atakayenusurika iwapo
itathibitika kuwa alishiriki kwenye mauaji hayo.
Dk. Nchimbi ambaye muda mwingi wa mazungumzo hayo alijinasibu kuwa
muumini mzuri wa utawala wa sheria, aliwataja wajumbe wa tume hiyo kuwa
ni wanahabari Pili Mtambalike kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT) na
Theophil Makunga kutoka Jukwaa la Wahariri (TEF) ambaye pia ni Mhariri
Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication inayochapisha magazeti ya
Mwananchi na Mwanaspoti.
Wengine ni Kanali Wema W. Wapo ambaye ni mtaalamu wa milipuko kutoka
Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na
Tathmini, Naibu Kamishna wa Polisi, Issaya Mungulu na Mwenyekiti wa tume
hiyo Jaji Mstaafu Pivel Ihema.
“Tume hii itafanya kazi zake kwa uhuru na iwapo wataona wataalamu wa
hapa ndani wameshindwa jambo fulani wasisite kutueleza… serikali
itautafuta utaalamu huo kutoka nje ya nchi.
“Ninaomba kuwahakikishia Watanzania kwamba askari yeyote atakayeguswa
na tume hii hatabaki salama, sikubaliani na dhuluma hasa ya vifo vya
raia na sipuuzi malalamiko yao,” alisisitiza Dk. Nchimbi huku akikwepa
kujibu baadhi ya maswali ya waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa waziri huyo, hadidu hizo za rejea zimetokana na taarifa
iliyotolewa na Jukwaa la Wahariri ambayo ni kujua chanzo cha kifo cha
Mwangosi, ukweli kuhusu uhasama kati ya polisi wa mkoani Iringa na
waandishi wa huko.
Aliitaka pia tume hiyo kueleza iwapo kuna orodha ya waandishi wa
habari watatu mkoani Iringa wanaowindwa na polisi, na usahihi wa nguvu
ya polisi iliyotumika kuwadhibiti wafuasi wa CHADEMA.
Jukumu lingine la tume hiyo ni kueleza kwa kina utaratibu wa vyama vya
siasa kukata rufaa pale vinapohisi kutotendewa haki na kama kweli kuna
uhusiano mbaya kati ya polisi na vyama vya siasa hasa wapinzani.
Kwa msisitizo Dk. Nchimbi alisema vurugu zilizofanyika Iringa ni
matokeo ya kuongezwa kwa muda wa kazi ya sensa ya watu na makazi ambapo
Jeshi la Polisi liliwazuia wanasiasa wote kufanya mikutano ya hadhara.
Hata hivyo, waziri huyo alishindwa kutoa ufafanuzi wa mkutano wa
uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo huko Bububu visiwani Zanzibar
ambapo Makamu wa Rais, Dk. Gharib Bilali, alishiriki.
Waziri huyo alisema serikali inajiuliza iwapo suala la sensa si muhimu
kwa CHADEMA kiasi cha kushindwa kuvumilia kwa siku saba za nyongeza.
Katika hali inayoonyesha waziri kukosa hisia na kuguswa na ukatili wa
jeshi lake, aliilaumu CHADEMA kwamba ndiyo iliyosababisha mauaji hayo.
“Hivi CHADEMA wanajisikiaje katika kipindi cha miezi mitatu kwenye
mikutano yao mitatu wamesababisha vifo vya watu watatu, familia za
marehemu hao zinawachukuliaje… unajua harakati za siasa hawakuanza wao,
Mwalimu Nyerere aliutafuta uhuru wa nchi hii kwa miaka saba bila kumwaga
damu (Tangu 1954 hadi 1961) tena akiwa na serikali ya kikoloni,”
alisema.
Amshukia IGP Mwema, Dk. Slaa
Katika kile alichokiita kumshangaa IGP Mwema, Dk. Nchimbi alisema
haelewi sababu za kiongozi huyo wa polisi kuendelea kumwacha huru Katibu
Mkuu wa CHADEMA, Dk. Slaa, wakati ametoa vitisho vilivyosababisha
mauaji ya mwandishi huyo.
Akizungumzia vitisho vya katibu huyo aliyewahi kugombea urais mwaka
2010, waziri huyo aliwaonyesha waandishi wa habari ujumbe mfupi wa simu
ya mkononi aliotumiwa IGP Mwema kutoka kwa Dk. Slaa.
Ujumbe huo ulisomeka hivi: ‘IGP nasubiri simu yako wajulishe polisi
wako waandae risasi za kutosha, mabomu ya kutosha. Mtakuwa na karamu ya
mauaji na kisha kusherehekea, mjiandae kwa kwenda mahakama ya The Hague.
Ni afadhali tufe kuliko manyanyaso haya. Dk. Slaa.’
Kutokana na ujumbe huo huku akizungumza kwa mafumbo, kauli ya Dk.
Nchimbi ni kumtaka IGP kumkamata Dk. Slaa na kumfikisha mahakamani kwa
madai ya kutoa vitisho na kusababisha mauaji.
“Namshangaa IGP Mwema mtu anatoa vitisho lakini hapelekwi mahakamani,
mtu ametuma ujumbe kama huu halafu anarudi nyumbani kwake analala…
anaendelea kuwa huru.
“Lakini zaidi namshangaa Dk. Slaa licha ya vitisho hivyo na kifo cha
mwandishi, bado hajaenda kujisalimisha polisi,” alisema waziri huyo
alipoulizwa hatua anazochukua baada ya IGP kukaa kimya licha ya ujumbe
aliotumiwa na Dk. Slaa.
Kwa mujibu wa waziri huyo wakiwa kwenye kikao Agosti 28 mwaka huu, IGP
Mwema alitumia muda mwingi kumwomba Dk. Slaa asitishe mikutano ya
hadhara kupisha shughuli za sensa jambo lililofikia muafaka kwa wawili
hao.
“Nilimsikia IGP akiongea kwa upole… ‘nakuomba kaka yangu Slaa nielewe
ndugu yangu nakuomba’ naamini waliafikiana,” alisema Dk. Nchimbi.
Akiendelea Nchimbi alisema; “Nikiwa waziri mwenye dhamana ya kusimamia
jeshi hili na kuona haki inatendeka polisi wanaodhulumu raia
hawatasalimika hata kidogo, nitawashughulikia nanyi mtaona hebu nipeni
miezi minne hivi.
“Baada ya tume hii mtaona… tangu niingie kwenye wizara hii nimeshaunda
tume tatu ambazo matokeo yake nitayatoa hivi karibuni,” alisema Dk.
Nchimbi na kuongeza kuwa hakuna waziri mpenda haki kama yeye na wananchi
hawatampata wa kufanana naye.
“Mtampata wapi waziri kama mimi…(wote kicheko),” alisema waziri huyo
ambaye kabla ya kupewa wizara hiyo alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni
na Michezo aliyewaahidi waandishi kusimamia upatikanaji wa sheria mpya
ya vyombo vya habari jambo lililokwama.
Alisema milango ipo wazi kwa raia kupeleka malalamiko yao huku
akisisitiza kwamba hana tabia ya kupuuza kero za wananchi zinazowagusa
askari polisi.
Katika hatua nyingine, Askofu wa Kanisa Kiinjili la Kilutheri (KKKT),
Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa amesema anasikitishwa
kuona raia wakiendelea kuuawa na polisi bila kuchukuliwa hatua.
Dk. Malasusa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Utetezi wa masuala ya
Kiuchumi, Haki za Binadamu na Utunzaji wa Uumbaji, alisema hali hiyo
inahatarisha amani na utulivu nchini.
“Inashangaza kuona uhai wa mwanadamu ambao ni zawadi kutoka kwa Mungu
unakatishwa kikatili tena katika mazingira yasiyoashiria hatari,”
alisema.
Alisema KKKT inaitaka serikali kukomesha mauaji ya aina hiyo
yasiendelee na polisi wazingatie maadili katika utekelezaji wa majukumu
yao.
Taarifa hii imeandaliwa na Irine Mark na Efracia Massawe Dar, Joseph Senga, Iringa na Christopher Nyenyembe, Rungwe.
Chanzo cha habari Tanzania Daima(05/09/2012)
No comments:
Post a Comment