JANA Kamati mbili zilizoundwa kuchunguza mauaji ya Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Televisheni cha Chanel Ten yaliyotokea Septemba 2, mkoani Iringa Daudi Mwangosi zilitoa matokeo yao.
Tunazipongeza kamati zote mbili kwa kazi kubwa walioifanya, zimetoa mapendekezo ambayo baadhi yake tunadhani yakifanyiwa kazi yanaweza kuleta mabadiliko.
Pamoja na kwamba Kamati zote mbili zinatofautiana katika maoni na ushaur, lakini hata hivyo zimeshindwa kueleza kiini kwa kuogopa kuingilia mwenendo wa kesi ilioko mahakamani inayomkabili askari anayedaiwa kumuua Mwangosi.
Pamoja na baadhi ya mapendekezo mazuri yaliyotolewa na kamati hizi, hasa ile ya iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, bado imeacha maswali mengi kuliko majibu.
Maswali hayo yanatokana na Kamati kushindwa kuweka hadharani ripoti ya kiini cha mauaji hayo ya kinyama yaliyofanywa na baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi kutokana na kesi hiyo ya Mahakamani ingawa ripoti tumeelezwa hiyo ipo.
Siku tatu baada ya Mwangosi kuuawa kikatili, Waziri wa Mambo ya Ndani, Nchimbi aliwaeleza Waandishi wa habari kuwa atalishughulikia suala hilo kwa haraka na kuhakikisha wale wote waliohusika wanafikishwa mahakamani.
Siku mbili kabla ya maandamo ya Waandishi wa Habari kulaani mauaji hayo, Nchimbi aliwatia moyo waandishi wa habari na tayari alikuwa amekwishaunda Kamati ya kuchunguza mauaji hayo.
Sisi Tanzania Daima Jumapili, tunahoji kama Nchimbi alifahamu kwamba matokeo ya ripoti ya Kamati kuhusu kiini cha kifo cha Mwangosi haiwezi kuwekwa hadharani, alikuwa na haja gani ya kuunda kamati hiyo?
Kama kweli pia alikuwa na dhamira ya dhati katika kulishughulikia jambo hilo, kwa nini mtu anayedaiwa kumuua Mwangosi alifikishwa mahakamani na kisha siku chache baadae akaunda kamati?
Kwa jinsi tunavyofahamu mwenendo wa kesi za mauaji huwa zinachukua muda mrefu hadi kuja kumalizika.
Zipo kesi ambazo tumeziona zimechukua miaka mitano hadi nane. Je ripoti hiyo ambayo imefichwa itatolewa baada ya miaka hiyo kesi kuisha?
Matokeo ya ripoti ya Kamati yametufanya tupate mashaka kwamba kulikuwa na mkakati wa wazi wa kuunda kamati wakati wakijua huko mbele isingeeleza kiini kwa sababu ya kesi iliyoko mahakamani.
Kamati imesema haiwezi kuweka hadharani ripoti hiyo nyingine kwa kuogopa kutumiwa kama ushahidi mahakamani. Tunajiuliza kama kamati hii iliundwa kwa dhamira ya dhati, kwa nini waogope? Je wametoa ripoti ya uongo?
Tunasema hivyo kwa sababu, Hakimu au Jaji hafikii kutoa uamuzi kwa kuongozwa na maneno ya kusikia mtaani, bali anaongozwa na weredi wake wa kuchambua mambo kwa misingi ya sheria kwa kuzingatia hoja zilizowasilishwa mbele yake na pande zote.
Kwetu Tanzania Daima, kama chombo hur, tuna kila sababu ya kuhoji kulikuwa na haja gani ya Kamati hiyo kupewa jina ‘Kamati ya kuchunguza mauaji ya Mwangosi’ kama nia ilikuwa ni kutoa mapendekezo na kusema nini kifanyike na si kuweka hadharani kiini kizima na hata kuorodhesha wanaopaswa kuwajibika.
Kama kamati hiyo iliundwa kwa ajili ya kuweka hadharani ripoti ya mapendekezo na si kutafuta kiini cha mauaji basi ingepewa jina la ‘Kamati ya kumshauri Waziri/serikali kuhusu mauaji ya Mwangosi.’
Majibu na matokeo ya namna hii inaifanya jamii ipoteze imani na kamati na tume kadhaa zinazoundwa kuchunguza mauaji na masuala mengine yaliyoigusa jamii moja kwa moja kama hili la mauaji ya Mwangosi.
Athari ya matokeo ya namna hiyo ni nyingi kwa jamii, ikiwamo kupoteza imani na vyombo vya vyombo vya serikali, hali inayoweza kuwafanya wananchi kujichukuliwa sheria mkononi.
Tunamaliza maoni yetu kwa kuishauri serikali kwamb, kama kweli ina nia ya dhati katika kushughulikia matukio makubwa kama hayo, kamwe isifanye mchezo danganya toto.
No comments:
Post a Comment