NANI KUTWAA TAJI? Ndilo swali kubwa wanalojiuliza Watanzania wengi wakati warembo 30 watakapopanda jukwaani katika ukumbi wa hoteli ya Blue Pearl, iliyopo Ubungo Plaza, Dar es Salaam kuwania taji la Redd’s Miss Tanzania 2012 kesho.
Na Mwandishi Wetu
Swali kubwa ambalo kila mtu anajiuliza ni mrembo yupi kati ya hao 30 ambaye atafanikiwa kutwaa taji hilo linaloshikiliwa na Salha Israel, huku watano kati yao wakiwa na uhakika wa kuingia hatua ya 15 Bora.
Warembo watano waliofanikiwa kupenya katika hatua hiyo ni Lucy Stephano aliyeshinda Miss Photogenic, Mary Chizi aliyetwaa taji la Miss Sports Lady, Babylove Kalala aliyeshinda Miss Talent, Magdalena Roy aliyetwaa taji la Top Model na Miss Personality, Happiness Daniel.
Mrembo atakayefanikiwa kutwaa taji la Redd’s Miss Tanzania 2012 atajitwalia kitita cha Sh milioni 8, pamoja na gari, huku washindi wengine wanaofuatia nao wakipata zawadi za kila aina.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino Agency, Hashim Lundenga, ambao ndio waandaaji wa Redd’s Miss Tanzania 2012, alisema washiriki hao watakuwa na kazi ngumu ya kuwania taji pamoja na zawadi hiyo.
Kwa mujibu wa waandaaji, mshindi wa pili atapata Sh milioni 6.2 wakati wa tatu akijinyakulia Sh milioni 4, mshindi wa nne ataondoka na Sh milioni 3 huku wa tano atatwaa Sh milioni 2.4, mshindi wa sita hadi 15, kila mmoja atajinyakulia Sh milioni 1.2 na washiriki wengine wote waliobaki kila mmoja atajipoza kwa Sh 700,000.
Kwa upande wake, Meneja wa Redd’s Original, Victoria Kimaro, alisema huu ni wakati sahihi wa kumpata mshindi bomba mwenye vigezo, hivyo aliwataka wapenzi wote wa tasnia ya urembo na wapenda maendeleo wote nchini, wajiandae kushuhudia fainali zilizokwenda shule.
“Kwa kweli shindano la mwaka huu tunatarajia litafana sana, hasa kwa kuzingatia kuwa, maandalizi yote yamekamilika kwa kiwango kikubwa na sisi tutahakikisha kuwa, mwaka huu kila atakayefika siku ya fainali anakuwa na jambo la kusimulia, kwa sababu ni shindano la kipekee,” alisema Victoria.
Mrembo atakayetwaa taji hilo ataiwakilisha Tanzania katika mashindano ya dunia yatakayofanyika mapema mwakani, huku akitegemewa kufanya makubwa zaidi kutokana na maandalizi atakayopewa.
Katika shindano hilo, kutakuwa na burudani za kila aina ikiwemo zile za ngoma za asili kutoka kwa msanii Wanne Star, pamoja na mkali wa muziki wa kizazi kipya Diamond Platinumz, pamoja na Winfrida Josephat ‘Rachel’.
Shindano la Redd’s Miss Tanzania 2012 linadhamiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Redd’s Original na kiingilio kitakuwa Sh 100,000.
No comments:
Post a Comment