NDUGU zangu, hakuna anayeweza kuupinga ukweli kwamba, maisha ya
sasa ni magumu, ugumu ambao kama mtu atabweteka na kushindwa kutimiza
wajibu wake ipasavyo upo uwezekano mkubwa wa kujikuta anaingia katika
mfumo wa maisha yasiyokuwa na mbele wala nyuma na ugumu huo wa maisha
kwake kuwa mara mbili yake.
Lakini licha ya ukweli huo, bado nafasi zipo wazi kwa watu kuingia katika ulimwengu wa mafanikio.
Lakini licha ya ukweli huo, bado nafasi zipo wazi kwa watu kuingia katika ulimwengu wa mafanikio.
Hii itatokea tu kama mtu ataamua kupambana ipasavyo na kuhakikisha haingii katika kapu la umaskini ambalo limejaa wengi hata wasiostahili kuwemo ndani yake.
Wapo watu na afya zao, nguvu za kutosha pamoja na maarifa waliyopewa na
Mungu lakini bado wameridhika kuishi maisha ya kifukara huku wakitegemea misaada kutoka kwa watu wengine ili kuweza kusogeza siku.
Hakika hii ni hatari sana na uhatari huo unakuja hasa pale unapomuona mtu ambaye ana kila sababu ya kuwa miongoni mwa watu wenye mafanikio lakini yeye anaona HAWEZI kuwa hivyo huku akiwa na dhana kwamba, yeye ni miongoni mwa wale waliopangiwa kuishi maisha ya kifukara hadi mwisho wa maisha yao.
Wapo wanaoamini kwamba, Mungu kaleta ulimwenguni watu wa aina mbili. Yaani kuna maskini ambao hata wafanye nini hawawezi kuwa matajiri na kuna matajiri ambao wao wamepangiwa neema ‘mwanzo mwisho’.
Watu wanaofikiria hivyo wapo huko mtaani, yaani wao
wanaamini wameumbwa na umaskini na hawawezi kufanya chochote
kitakachoweza kuwabadilisha kuwa miongoni mwa matajiri. Wenye dhana kama
hizi ndiyo wale tunaowaona huko mtaani wakiishi maisha wasiyostahili
kuishi.
Mtu kama ni kilema asiye na mikono wala miguu, anaweza kuwa sahihi akisema hana kitu anachoweza kukifanya akawa tajiri kutokana udhaifu aliokuwa nao lakini wewe ambaye umejaaliwa kuwa miongoni mwa waliojaaliwa kuwa na viungo kamili, nguvu pamoja na maarifa iweje ujione kwamba uko sawa kuishi maisha duni?
Huoni kwamba utakuwa unajidhalilisha na kumkosea Mungu wako? Ifike wakati ukae chini na ujiulize sababu za wewe kuendelea kuishi maisha mabaya wakati wenzako kila siku wanapiga hatua mbele.
Huenda kuna sehemu unakosea hivyo ni vyema ukaibaini na kufanya mabadiliko ya haraka ili na wewe uweze kuwa miongoni mwa wale waliotumia vizuri nafasi zao za kuletwa hapa ulimwenguni.
Kama unataka kutimiza wajibu wako wa kuletwa hapa ulimwenguni una kila sababu ya kufanya kazi kwa bidii bila kuridhika na hicho kidogo unachokipata sasa. Siku zote ota kuwa miongoni mwa matajiri wakubwa duniani bila kujali kwa sasa uko katika nafasi gani.
Nasema hivyo kwa sababu, kuna wanaodhani kwamba kwa kuwa sasa hivi ni masikini watakuwa wamechelewa na uwezekano wa wao kuwa matajiri haupo tena. La hasha!
Siku zote mbio za kuelekea kwenye utajiri huanzia kwenye mstari wa umaskini kwa maana hiyo, hapo hapo ulipo anza kukimbia kwa spidi kubwa huku ukiwa na malengo ya kuwa wa kwanza kuuvuka mstari wa kuingia kwenye mafanikio.
Niseme tu kwamba, maisha ni malengo, maisha ni kupanga na kuchagua. Panga mfumo sahihi wa maisha yako lakini pia chagua mafanikio. Tuonane tena wiki ijayo. kwa mada nyingine hapa.
No comments:
Post a Comment