WAKAZI wa wilaya ya Bukombe, mkoani Geita, wameilalamikia
hospitali ya wilaya hiyo kutokana na kukithiri kwa vitendo vya rushwa na
kusababisha wagonjwa wengi kukosa huduma za matibabu.
Wakazi hao walitoa malalamiko hayo juzi kwa nyakati tofauti
walipokuwa wakiwasilisha kero zao kwa mbunge wa Bukombe, Profesa
Kulikoyela Kahigi (CHADEMA), alipofanya ziara jimboni humo ili
kusikiliza kero za wananchi.
Walidai baadhi ya watumishi hospitalini hapo wamekuwa na tabia ya
kuomba rushwa, ili waweze kuwapatia huduma za matibabu na dawa wagonjwa.
Kwa upande wao kinamama wa kijiji cha Kagwe, walisema pamoja na huduma
kwa mama mjamzito na watoto chini ya miaka mitano kuwa bure, wamekuwa
wakitozwa fedha, ili waweze kupatiwa huduma ya matibabu.
Aidha, kinamama hao walilalamikia kitendo cha kuuziwa kadi za kiliniki kati ya sh 500 hadi 1,500.
Walisema kutokana na vitendo hivyo, baadhi ya kinamama hulazimika kujifungulia majumbani.
Mbali ya hilo, walidai baada ya mama kujifungua anapotaka kuchukua cheti cha kuzaliwa cha mtoto hulazimika kutoa sh 3,500.
Akijibu kero hizo, Profesa Kahigi alisema alishawaeleza watumishi wa
halmashauri husika pamoja na kuwasilisha kwa Waziri Mkuu kuhusu tatizo
hilo.
“Ndugu zangu niwaambie nchii hii watu wanakufa kutokana na mfumo mbaya
wa uongozi ambao umejaa ufisadi. Mtu anajali maslahi yake binafsi na
kuwaacha wenzake wafe,” alisema.
Kaimu Mganga Mkuu, Dk. Joshua Mazingo, alisema inawezekana tatizo hilo lipo kwa baadhi ya watumishi wasio waaminifu.
Hata hivyo, alisema huduma ya dawa na vifaa tiba katika hospitali nyingi ikiwemo hospitali hiyo ni tatizo kubwa.Kuhusu kuuziwa kadi, alisema siyo haki kwani zote zinapaswa kutolewa bure.
Habari na Danson Kaijage
No comments:
Post a Comment