Taasisi
ya Kimataifa inayorithi Kazi za Mahakama za Umoja wa Mataifa (MICT)
imewaachia huru kabla ya muda wao wa adhabu kuisha, watu wawili
waliokuwa wanatumikia kifungo baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994.
Watu hao ni pamoja na meya wa zamani wa wilaya ya Gikongoro, mkoa wa Kigali Vijijini, Paul Bisengimana na kiongozi wa zamani wa wanamgambo wa Interahamwe mkoani Gisenyi, Omar Sereshago. Wawili hao walikuwa wanatumikia adhabu zao nchini Mali.
Wakati anaachiwa,Bisengimana
alikuwa ameshatumikia theluthi mbili ya kifungo cha miaka 15
alichopewa.Alikuwa kizuizini tangu Desemba 4, 2001.
Meya huyo alitiwa hatiani Aprili
13, 2006 kwa kusaidia na kuunga mkono kutendeka kwa uhalifu wa kuua na
kuteketeza kizazi kama uhalifu dhidi ya binadamu baada ya yeye mwenyewe
kukiri makosa hayo.
Serushago kwa upande wake
ameachiwa akiwa ameshatumikia robo tatu ya kifungo cha miaka 15 jela
alichopewa Februari 5, 1999 baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya
kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu. Kiongozi huyo wa wanamgambo
alikuwa kizuizini tangu Juni 9, 1998. Yeye pia kama alivyo mfungwa
mwenzake alikiri kwa hiari yake mashitaka hayo dhidi yake.
Katika uamuzi uliomhusu
Bisengimana, Rais wa MICT, Jaji Theodor Meron alisema, ‘’Baada ya
kuchambua kwa makini vipengele vilivyomo katika sheria na pia mazingira
maalum ya kesi ya Bisengimana, nimeonelea kwamba anastahili kuachiwa
huru mapema na mara moja.’’ Alimwelekeza Msajili kuifahamisha serikali
ya Mali juu ya uamuzi huo.
Uamuzi wa MICT ambayo ilianzishwa
rasmi 2010 kurithi kazi za mahakama mbili za Umoja wa Mataifa ikiwa ni
pamoja na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) na
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu katika Yogoslavia ya zamani (ICTY)
imeonekana kutatua mgogoro wa kisheria wa muda mrefu kati ya mahakama
hizo mbili juu ya suala hilo.
Katika ICTR, mfungwa anatakiwa
kutumikia robo tatu ya adhabu aliyopewa kabla ya kufikikiriwa kuachiwa
huru mapema wakati ICTY, uamuzi kama huo unaweza kutolewa iwapo mfungwa
atakuwa ameshatumikia theluthi mbili ya adhabu yake.
Lakini katika uamuzi wake, Rais
Meron alisema ‘’Nimeonelea kwamba wafungwa wote wanaosimamiwa na MICT
wanastahili kutendewa sawa.’
No comments:
Post a Comment